Mar 15, 2021 11:26 UTC
  • Syria: Muongo mmoja baada ya kuanza vita vya kimataifa vya kigaidi

Umetimia muongo mmoja tokea vianze vita baina ya serikali ya Syria na makundi ya kigaidi. Swali muhimu ambalo linaibuka hapa ni hili, je ni kwa nini vita hivi vilianza na vimekuwa na matokeo gani baada ya kupita miaka 10.

Syria sawa na nchi nyingi za Kiarabu ilishuhudia maandamano ya wananchi mwaka 2011. Lakini kuna sababu iliyopelekea matukio ya Syria yachukue muelekeo wa kimataifa. Syria ni kati ya nchi ambazo kwa muda mrefu zimekuwa karibu na harakati za muqawama au mapambano ya Kiislamu katika eneo hasa kadhia ya ukombozi wa Palestina. Kwa msingi huo, punde baada ya maandamano kuanza, kulitekelezwa njama ya kimataifa ya kuipindua serikali iliyoko madarakani Syria kwa lengo la kuileta madarakani serikali kibaraka ambayo ingeenda sambamba na matakwa ya Magharibi ya kutaka nchi za eneo la Asia Magharibi ziwe na uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel. Ili kufikia lengo hilo maadui wa Syria waligeuza maandamano ya kawaida ya wananchi kuwa vita baina ya mfumo wa nchi hiyo na makundi ya kigaidi yaliyokuwa yakiungwa mkono na madola ya Magharibi, utawala wa Kizayuni wa Israel, baadhi ya tawala za Kiarabu na Uturuki.

Lengo la kuibuliwa vita dhidi ya Syria lilikuwa ni kuhakikisha kuwa, baada ya kupinduliwa madikteta huko Tunisia, Misri, Libya na Yemen, ambao walikuwa waitifaki wa Magharibi, mlingano wa nguvu katika eneo usibadilike na kuwa kwa maslahi ya harakati za muqawama.

Baada ya muongo mmoja tokea kuanza maandamano na kisha vita vya ndani nchini Syria, mfumo unaotawala chini ya uongozi wa Rais Bashar Assad umebakia madarakani. Mhimili wa muqawama umeweza kuonyesha nguvu na uwezo wake wa kukabiliana na makundi ya kigaidi yaliyokuwa na magaidi kutoka zaidi ya nchi 80. Mhimili wa muqawama umefanikiwa pia kukomboa asilimia 90 ya ardhi ya Syria ambayo ilikuwa inakaliwa kwa mabavu na magaidi. Harakati za hivi karibuni za Marekani na Uturuki katika kuunga mkono baadhi ya makundi ya kigaidi na kupora utajiri wa mafuta ghafi ya petroli ya Syria ni jambo linaloashiria lengo halisi la kuibuliwa mgogoro wa Syria.

Rais Assad wa Syria akiwa na majenerali wa jeshi la nchi hiyo wakipanga mkakati wa kukabiliana na magaidi

Pamoja na hayo, nukta muhimu zaidi ya vita hivi vya kimataifa ni kadhia ya ubinadamu. Mgogoro wa Syria umepelekea kuibuka maafa makubwa ya kibinadamu. Katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, zaidi ya Wasyria 380,000 wameuawa vitani na malaki ya wengine wamejeruhiwa. Aidha vita vya Syria vimepelekea watu milioni 12 kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi hiyo. 

Fabrizio Carboni Mkurugenzi wa Shirika la Msalaba Mwekundu katika eneo la Asia Magharibi anasema hivi kuhusu kadhia hii: "Moja kati ya mambo ya kushtua katika utafiti wetu ni kuwa tulifahamu kuwa katika kila Wasyria sita, mmoja alipoteza wazazi wake au wamejeruhiwa. Aidha nusu ya Wasyria wamepoteza jamaa katika familia au rafiki. Hali kadhalika karibu watoto 12,000 wameuawa au kujeruhiwa tokea mwanzo wa vita vya Syria. Aidha mbali na hayo, janga la Syria limesababisha matatizo mengi ya kisaikolojia kwa familia za waliouawa, kujeruhiwa au kuathirika kwa njia moja au nyingine na vita hivyo. 

Watoto ni waathirika wakubwa zaidi wa vita vya Syria. Christian Schneider mkurugenzi wa Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Watoto (UNICEF) nchini Ujerumani anasema hivi kuhusu nukta hiyo: "Baada ya muongo mmoja wa vita, hali ya watoto nchini Syria ni mbaya zaidi kuliko wakati wowote ule. Idadi kubwa ya watoto wamelazimika kufanya kazi ili wabakie hai." Naye Ted Chaiban, Mkurugenzi wa UNICEF Mashariki ya Kati (Asia Magharibi) na Afrika Kaskazini anasema: "Takribani asilimia 90 ya watoto wa Syria wanahitaji misaada ya kibinadamu. Mbali na hayo, mgogoro wa Syria umepelekea kuibuka maafa makubwa zaidi katika mfumo wa elimu na masomo katika historia ya sasa. Karibu watoto milioni 2.5 nchini Syria na wengine 750,000 wanaoishi kama wakimbizi katika nchi jirani hawaendi shuleni." Kwa mujibu wa tathmini, hivi sasa karibu Wasyria nusu milioni wanakabiliwa na lishe duni.

Magaidi wakufurishaji wa ISIS waliovamia Syria kwa himaya ya madola ya kigeni

Mbali na hayo, mfumo wa jadi wa kimaisha wa watu wa Syria umetoweka kutokana na vita. Biashara za watu zimevurugika, mfumuko wa bei, ukosefu wa ajira na umasikini ni kati ya matatizo yanayowakumba watu wa Syria. Aidha karibu thuluthi moja ya watu wa Syria hawawezi kukidhi mahitaji yao ya kimsingi.

Hali kadhalika Khaled Hboubati, mwenyekiti wa Hilali Nyekundu ya Syria anasema hivi kuhusu vita nchini humo:"Kuendelea mapigano, hali mbaya ya kiuchumi, mgogoro wa wakimbizi na janga la COVID-19 yote ni mambo yanayoashiria kuwa Wasyria wangali wanakabiliwa na matatizo na masaibu. Zaidi ya Wasyria milioni 13 wanahitaji msaada  ingawa si mkubwa kuweza kukidhi mahitaji yao ya kimsingi. Aidha Wasyria karibu milioni 8 wanahitaji msaada kikamilifu ili kukidhi mahitaji yao ya kimaisha. Fauka ya hayo,Wasyria waliowengi wanakabiliwa na ukosefu wa usalama wa chakula. Karibu Wasyria milioni 12.4 au asilimia 60 ya Wasyria hawapati chakula cha kutosha na inaaminika kuwa karibu asilimia 90 ya Wasyria wanaishi chini ya mstari wa umasikini."

Hayo ni matokeo ya vita dhidi ya Syria ambavyo vilianzishwa na makundi ya kigaidi kwa uungaji mkono wa Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya na kwa ushirikiano wa Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu, Uturuki na utawala wa Kizayuni wa Israel. Uwepo wa madola makubwa katika vita dhidi ya Syria ni jambo ambalo limepelekea Umoja wa Mataifa usiweze kuchukua hatua za kivitendo za kuhitimisha vita au kupunguza mgogoro wa Syria.

 

Tags