Mar 16, 2021 12:27 UTC
  • Waziri Mkuu wa Iraq atoa hotuba kwa mnasaba wa kumbukumbu ya mashambulizi ya Halabcha

Waziri Mkuu wa Iraq amesema kuwa kuadhimisha kumbukumbu ya mashambulizi ya kemikali yaliyotekelezwa katika mji wa Halabcha katika eneo la Kurdistan huko Iraq kunakumbushia kuuliwa maelfu ya raia na watu wasio na hatia wa eneo hilo.

Mustafa al Kadhemi amesema kuwa machungu ya msiba huo uliosababisha vifo vya maelfu ya raia yanaendelea hadi leo ili kutufahamisha ni masaibu na madhara gani yanayowaathiri wanadamu wakati silaha za maangamizi ya halaiki zinapoangukia katika mikono ya dhalimu. Waziri Mkuu wa Iraq ameyasema hayo katika maadhimisho ya kukumbuka kutimia  mwaka wa 33 tangu kujiri mashambulizi ya kinyama ya kemikali katika mji wa Halabcha huko Kurdistan Iran yaliyofanywa na utawala wa Baath.  

Al Kadhemi ameongeza kuwa, watu wa Kurdistan walikuwa wahanga wa maafa hayo ya Halabcha; sawa kabisa na wananchi wa Iraq  walivyojitolea kwa jaili ya kupigania kuwa huru nchi yao na kujitoa katika makucha ya ukandamizaji wa mtawala dhalimu. Lakini leo hii  tutafanya kila linalowezekana ili kujifunza na kupata ibra kutoka kwa mashahidi waliojitolea   ili kuijenga Iraq iliyo huru na ya kidemokrasia.  

Utawala wa Saddam Hussein dikteta wa zamani wa utawala wa Baath huko Iraq tarehe 16 mwezi Machi mwaka 1988 aliamuru kutekelezwa mashambulizi ya kemikali dhidi ya wakazi wa maeneo ya mji wa Halabcha Kurdistan nchini humo. Watu karibu 5000 wa Halabcha waliuawa na wengine karibu ya 7,000 hadi 10,000 walijeruhiwa katika hujuma hiyo ya kemikali huko Halabcha. Aidha mamia ya watu waliaga dunia kutokana na mdhara ya kemikali, magonjwa na ulemavu wa mwili waliozaliwa nao miaka kadhaa baada ya shambulio hilo. 

Shambulio la kemikali la Halabcha nchini Iraq 

 

Tags