Mar 20, 2021 09:39 UTC
  • Uturuki: Israel ni mkiukaji wa sheria za kimataifa

Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki imesema mpango wa utawala wa Kizayuni wa Israel wa kupora ardhi na kubomoa nyumba za Wapalestina unakanyaga wazi sheria za kimataifa.

Katika taarifa iliyonukuliwa na shirika la habari la Anadolu, wizara hiyo imebainisha kuwa, mpango huo wa utawala ghasibu wa Israel utakaowaacha bila makazi mamia ya Wapalestina hususan wakazi wa mashariki mwa Quds tukufu unaonesha azma ya Tel Aviv ya kuendelea kughusubu na kukalia kwa mabavu ardhi za Wapalestina badala ya kufuata mkondo wa amani.

Taarifa hiyo ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki imeongeza kuwa,  utawala huo pandikizi unachukua hatua hii wakati huu ambapo Palestina inajaribu kukabiliana na makali ya janga la corona.

Imeitaka jamii ya kimataifa kusimama na wananchi wa Palestina kupinga sera hiyo ya Wazayuni ya kunyakua ardhi za Wapalestina na kubomoa nyumba zao.

 

Bomoabomoa ya Wazayuni huku Palestina inayokaliwa kwa mabavu

Kwa mujibu wa azimio nambari 2334 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, shughuli za ujenzi wa vitongoji unaofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel ni kinyume cha sheria, lakini pamoja na hayo utawala huo ghasibu unaendelea kubomoa nyumba za Wapalestina na kujenga vitongoji; lengo likiwa ni kubadilisha muundo wa idadi ya watu na wa kijiografia wa maeneo ya Wapalestina ili kuyayahudisha maeneo hayo na kuimarisha udhibiti wake.

Utawala wa Kizayuni wa Israel umeandaa mpango wa kubomoa nyumba zaidi ya 100 za Wapalestina katika mji unaoukalia kwa mabavu wa Baitul Muqaddas na kuwaacha Wapalestina wapatao 1,550 bila mahali pa kuishi.

 

Tags