Apr 03, 2021 09:43 UTC
  • Kamati ya pamoja ya Iran na Iraq yachunguza mauaji ya kigaidi ya Soleimani

Mkuu wa Baraza Kuu la Haki za Binadamu la Vyombo vya Mahakama vya Iran amesema faili la mauaji ya kigaidi ya Shahid Qassem Soleimani, aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran (IRGC) linafuatiliwa na kamati ya pamoja ya Iran na Iraq.

Ali Baqeri-Kani amesema hayo leo Jumamosi katika mahojiano na shirika la habari la Mehr na kubainisha kuwa, mchakato wa kuchunguza mauaji ya Jenerali Soleimani unafuatiliwa kwa kina na kwa kasi kubwa na kamati ya pamoja ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Iraq.

Ameeleza bayana kuwa, kufuatia kuundwa kamati hiyo ya pamoja baada ya Mkuu wa Vyombo vya Mahakama wa Iran kuitembelea Iraq hivi karibuni, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Iraq pamoja na Naibu wa Mwendesha Mashitaka Mkuu wa Tehran wameapa kulifuatilia kwa makini faili la mauaji hayo yaliyofanywa na wanajeshi magaidi wa Marekani mapema mwaka 2020 mjini Baghdad.

Afisa huyo wa Idara ya Mahakama ya Iran ameongeza kuwa, kamati hiyo itaendelea na uchunguzi wake huru, licha ya kuwa mauaji hayo yanapaswa kufuatiliwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu (ICJ). 

Mashahidi Soleimani na Abu Mahdi al-Muhandis

Mapema mwaka huu, Agnes Callamard, Ripota maalumu wa Umoja wa Mataifa alisema kuwa, mauaji ya kigaidi ya Hajj Qassem Soleimani ni kinyume na sheria za kimataifa na kuongeza kuwa, mauaji hayo yaliyofanywa na Marekani ni uvunjaji wa haki ya kujitawala Iraq.

Luteni Jenerali Qassem Soleimani, aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la SEPAH, aliuliwa kidhulma katika shambulio la kuvizia la anga lililofanywa na wanajeshi magaidi wa Marekani karibu na Uwanja wa Ndege wa Baghdad, mji mkuu wa Iraq, tarehe 3 Januari, 2020 akiwa uraiani tena akiwa mgeni rasmi wa serikali ya Iraq.

Tags