Apr 04, 2021 03:08 UTC
  • Jaribio la mapinduzi Jordan, makumi ya viongozi watiwa mbaroni + Video

Duru za habari usiku wa kuamkia leo zimetangaza habari ya kutiwa mbaroni makumi ya viongozi wa ngazi za juu wa Jordan kwa tuhuma za kujaribu kufanya mapinduzi dhidi ya mfalme Abdallah II.

Vyombo mbalimbali vya habari duniani vimeakisi habari hiyo na kusambaza pia mkanda mfupi wa video unamuonesha mrithi wa zamani wa kiti cha ufalme wa Jordan, Hamza bin Hussein akisisitiza kuwa amewekwa kwenye kifungo cha nyumbani yeye na walinzi wake.

Televisheni ya al Alam nayo imeweka mtandaoni mkanda huo wa video na kuandika kuwa, mrithi huyo wa zamani wa kiti cha ufalme wa Jordan amewalaumu viongozi wa nchi yake kwa kushindwa kuiongozi vizuri Jordan na kusema, inashanga kuona kuwa ukosoaji mdogo wa siasa za utawala umepelekea niwekwe kwenye kifungo cha nyumbani.

Shirika la habari la FARS limeripoti kuwa viongozi wasipungua 20 wa ngazi za juu pamoja na wakuu wa kikabila na watu wa familia ya kifalme wamewekwa chini ya ulinzi kwa kile kilichodaiwa ni tishio la usalama wa Jordan.

Televisheni ya al Jazeera imemnukuu mwanamfalme Hamza akisema kuwa, ametakiwa na mkuu wa jeshi la Jordan asitoke nje na asiwasiliane na watu na wala asionane nao.

Gazeti la Washington Post limenukuu duru za karibu na familia ya kifalme ya Jordan zikikanusha kuhusika mrithi huyo wa zamani wa kiti cha ufalme wa nchi hiyo katika jaribio la mapinduzi.

Televisheni ya al Mayadeen imeripoti kuwa, makumi ya viongozi wa ngazi za juu wa Jordan wamekamatwa katika kile kilichodaiwa ni kupanga njama za kuupindua utawala wa mfalme Abdullah II wa nchi hiyo.