Apr 07, 2021 12:13 UTC
  • Makundi ya Muqawama ya Iraq yatishia kushambulia vikosi vya majeshi ya Marekani

Makundi ya Muqawama na mapambano ya Iraq yametishia kutoa vipigo vikali na makini kwa majeshi vamizi ya Marekani yaliyoko nchini humo iwapo Baghdad na Wshington hazitatangaza muda maalumu wa kuondoka majeshi hayo katika ardhi ya Iraq. 

Taarifa hiyo imetolewa na Barza la Uratibu la Muqawama wa Iraq linalojumuisha harakati za mapambano za Kataib Hizbullah ya Iraq, Asaib Ahlul Haqq, Harakati ya Nujabaa na Batalioni ya Sayyidus Shuhadaa.  
Tishio hilo limetolewa masaa machache kabla ya kuanza duru ya tatu ya mazungumzo ya kistratijia baina ya serikali ya Baghdad na Washington yanayofanyika leo kujadili masuala muhimu likiwemo linalodaiwa ni "ushirikiano katika kupambana na ugaidi". 

Taarifa iliyotolewa na makundi hayo imesema: Hii leo Muqawama unalazimika kutoa jibu kali na vipigo vikubwa na makini iwapo mazungumzo ya Baghdad na Washington hayatajumuisha tangazo la wazi la tarehe ya kuondoka majeshi vamizi katika anga na ardhi ya Iraq. 

Taarifa hiyo imesema makundi ya Muqawama yana taarifa zinazosema kuwa, taarifa itakayotolewa baada ya mazungumzo ya leo kati ya serikali za Baghdad na Washington haitakuwa hata na ishara ya kutekelezwa agizo la Bunge la Iraq lililotaka kufukuzwa majeshi vamizi ya Marekani nchini Iraq. 

Itakumbuka kuwa tarehe 5 Januari mwaka 2020 Bunge la Iraq lilitoa azimio linaloitaka serikali kufukuza majeshi yote ya kigeni katika ardhi ya nchi hiyo. Agizo hilo lilitolewa baada ya jeshi gaidi la Marekani nchini Iraq kumua aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, Luteni Jenerali Qassem Soleimani na Kaimu Mamanda wa kikosi cha kujitolea cha wananchi wa Iraq, Abu Mahdi al Muhandis karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Baghdad. Kamanda Qassem Soleimani alikuwa nchini Iraq kwa ziara rasmi na kwa mwaliko wa aliyekuwa waziri mkuu wa nchi hiyo. 

Marekani ina zaidi ya wanajeshi 2,500 nchini Iraq. 

Tags