Apr 08, 2021 02:37 UTC
  • Tathmini ya kikao cha tatu cha Baghdad na washington

Duru mpya ya mazungumzo ya kistratijia baina ya Baghdad na Washington ilianza jana Jumatano kwa njia ya video. Taarifa iliyotolewa huko nyuma na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilisema kuwa mazungumzo hayo yatahusu usalama, namna ya kupambana na ugaidi, nishati na masuala ya kisiasa.

Duru mbili za mwanzo za mazungumzo hayo tayari zimefanyika kati ya pande mbili hizo. Duru ya kwanza ilifanyika mwezi Juni na ya pili mwezi Septemba mwaka uliopita kufuatia safari ya Mustafa al-Kadhimi, Waziri Mkuu wa Iraq mjini Washington Marekani.

Baada ya kufanyika duru ya pili ya mazungumzo, Donald Trump rais wawakati huo wa Marekani alitangaza kwamba askari wa nchi hiyo walioko Iraq wangeondoka baada ya miaka mitatu, jambo lililowakasirisha sana wabunge wa Iraq waliotaka sheria iliyopasishwa na bunge ya kutaka askari wote wa Marekani waondoke mara moja, itekelezwe haraka iwezekanavyo.

Bunge la Iraq lilipitisha sheria ya kufukuzwa nchini humo askari wa Marekani tarehe 5 Januari 2020, ikiwa ni siku mbili tu baada ya kuuliwa kigaidi na serikali ya Marekani, Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu na Abu Mahdi al-Muhandis, Naibu Mkuu wa Jeshi la Kujitolea la Wananchi wa Iraq la Al-hashdu-Sha'abi.

Qassem Soleimani (kushoto) na Mahdi al-Muhandis waliouawa kigaidi na askari wa Marekani

Hivi sasa duru ya tatu ya mazungumzo ya Baghdad na Washington inafanyika katika hali ambayo hakuna hatua yoyote muhimu iliyochukuliwa katika mwaka mmoja uliopita kwa ajili ya kuondolewa askari wa Marekani katika ardhi ya Iraq, na katika upande wa pili, hii ni mara ya kwanza kwa serikali ya muda ya Iraq kufanya mazungumzo na serikali ya Joe Biden wa Marekani aliyeingia madarakani tarehe 20 Januari mwaka huu.

Nukta muhimu katika mazungumzo ya Baghdad na Washington ni kwamba, kuna msimamo mmoja ndani ya Iraq kuhusu udharura wa kufukuzwa askari wa Marekani katika ardhi ya nchi hiyo, hata kama Marekani kwa upande wake inasema haiko tayari kuondoa askari wake katika nchi hiyo ya Kiarabu kwa kutilia maanani kwamba imegharamika pakubwa katika kuwaweka askari wake katika nchi hiyo.

Kwa msingi huo, licha ya kuwa mazungumzo hayo yanafanyika katika mtazamo mpana wa kuondolewa askari wa Marekani huko Iraq, lakini ni wazi kuwa mazungumzo hayo yataghubikwa na masuala mengine mengi yasiyo ya kuondolea askari hao wa kigeni.

Ni kutokana na ukweli huo ndipo Kati' ar-Rikabi, mwanachama wa Muungano wa Serikali ya Sheria wa Iraq akasema kuwa duru ya tatu ya mazungumzo ya kistratijia ya Iraq na Marekani itakamilisha duru nyingine mbili zilizopita za mazungumzo hayo. Amesema: Mazungumzo hayo hayatahusu tu suala la kuondolewa askari wa Marekani katika ardhi ya Iraq bali kama zilivyokuwa duru za kwanza na pili, yatahusu pia masuala ya usalama, uchumi, mafunzo, kilimo na vile vile umeme na mafuta.

Mustafa al-Kadhim, Waziri Mkuu wa Iraq

Muhammad Bazyani, Katibu Mkuu wa Harakati ya Marekebisho na Ustawi ya Kurdistan ya Iraq amesema kwamba kutokana na kuwa hadi sasa Marekani imeshindwa kufikia malengo yake nchini Iraq na eneo zima la Asia Mashariki, sasa inaona kwamba fursa iliyosalia ni kutumia mazungumzo ya kistratijia ya Iraq kwa ajili ya kubakisha askari wake nchini humo. Anasema hata kama haitafanikiwa kubakisha askari wake katika nchi hiyo kwa muda mrefu lakini itatumia mashirika yake makubwa kuendelea kuwa na ushawishi katika nchi hiyo.

Inaonekana kuwa Mustafa al-Kadhimi kwa uapande mmoja anajaribu kuyatumia mazungumzo hayo kujaribu kupunguza mashinikizo ya makundi ya Iraq yanayotaka kuondolewa mara moja askari wa Marekani katika ardhi ya nchi hiyo na kwa upande wa pili, apanguze kasi ya kuondoka askari hao ili kupata uungaji mkono wa Marekani kwa ajili ya kuendelea kubakia katika kiti cha uwaziri mkuu wa Iraq. Uchaguzi wa bunge la Iraq umepangwa kufanyika mwezi Novemba mwaka huu na al-Kadhimi anafanya juhudi kubwa za kuunda serikali ijayo ya kudumu ya nchi hiyo.

Tags