Apr 08, 2021 03:10 UTC
  • Amnesty: Israel inazuia kupelekwa chanjo ya corona kwa Wapalestina

Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limetangaza kuwa, hatua za kihasama za utawala wa Israel zinazuia operesheni ya kutumwa chanjo ya virusi vya corona huko Palestina.

Shirika la Amnesty International limesema katika ripotii yake ya kila mwaka kwamba, Israel imeendelea kukiuka sheria za kimataifa kwa kuzuia operesheni ya kupelekwa chanjo ya virusi vya corona kwa Wapalestina milioni tano wanaoishi Ukingo wa Magharibi na Ukanda wa Gaza. 

Hii ni licha ya kuwa, idadi ya waathirika wa virusi vya corona huko Palestina inaongezeka kwa kasi kutokana na vizuizi za utawala haramu wa Israel na uhasama wake dhidi ya Wapalestina. Hadi sasa Wazayuni wa Israel wanaendelea kuzuia hatua yoyote ya kupelekwa chanjo ya corona kwa raia wa Palestina. Viongozi wa utawala haramu wa Israel wametangaza kuwa, hawataruhusu kuingizwa chanjo hiyo katika eneo la Ukanda wa Gaza.

Wakati huo huo makundi ya mapambano ya ukombozi wa Palestina yameitahadharisha Israel kutokana na hatua yake ya kuzuia chanjo ya corona kwa Wapalestina wa Ukanda wa Gaza. 

Taarifa iliyotolewa na makundi hayo imesisitiza kuwa, walimwengu hususan Shirika la Afya Duniani (WHO) wanapaswa kuushinikiza utawala wa Kizayuni wa Israel na kuulazimisha uruhusu kupeleka chanjo ya corona kwa watu wa Ukanda wa Gaza.  

Tags