Apr 08, 2021 13:21 UTC
  • Jeshi la Anga la Syria lafanikiwa kuzuia  hujuma ya Israel

Jeshi la Anga la Syria limetangaza kuwa Alhamisi asubuhi limefanikiwa kuzuia hujuma ya ndege za kivita za utawala wa Israel.

Shirika rasmi la habari la Syria SANA limesema Jeshi la Anga la Syria limefanikiwa kutungua makombora kadhaa kutoka Israel kabla hayajatua kusini mwa Damascus.

Kwa mujibu wa SANA, makombora hayo yalivurumishwa na ndege za kivita za utawala wa Kizayuni wa Israel ambazo zilikuwa zinatokea upande wa milima ya Golan ya Syria inayokaliwa kwa mabavu na utawala huo wa Kizayuni. Aidha ndege hizo vamizi za Israel pia zimejipenyeza Syria kupitia mpaka wa Lebanon.

Taarifa zinasema wanajeshi wanne wa Syria wamejeruhiwa katika hujuma hiyo.

Magaidi wa ISIS

Israel imekuwa ikishambulia vituo vya Jeshi la Syria mara kwa mara kwa lengo la kudhoofisha jeshi hilo na kuwaunga mkono magaidi wakufurishaji.

Mgogoro wa Syria ulianza mwaka 2011 wakati magaidi walipoivamia nchi hiyo kwa himaya ya Saudi Arabia na Marekani na waitifaki wao kwa lengo la kubadilisha mlingano wa kieneo kwa maslahi ya utawala wa Israel.

Jeshi la Syria limefanikiwa kulisambaratisha kundi la kigaidi la ISIS nchini humo kwa msaada wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Russia.