Apr 10, 2021 07:45 UTC
  • Hamas: Kukataa kushirikiana na ICC kunaonesha upeo wa kiburi cha Israel

Msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) amesema kitendo cha utawala wa Kizayuni wa Israel cha kukataa kutoa ushirikiano kwa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) kinaonesha wazi upeo wa jeuri na kiburi cha utawala huo haramu kwa taasisi za kimataifa.

Hazim Qassem amesema msimamo wa Israel wa kukataa kushirikiana na ICC umetokana na dhana ya utawala huo kwamba upo juu ya sheria na wala haupaswi kuwajibishwa wala kubebeshwa dhima.

Hivi karibuni, mahakama ya ICC ilianzisha uchunguzi kuhusu jinai za kivita zilizofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel katika ardhi za Palestina unazozikalia kwa mabavu.

Fatou Bensouda, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa ICC, Jumatano ya Machi 3 alitangaza habari ya kuanza uchunguzi wa mahakama hiyo juu ya jinai za kivita zilizofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel katika vita ulivyovianzisha huko Gaza mwaka 2014 na pia katika ujenzi wake wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni kwenye ardhi unazowapora Wapalestina za Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Baytul Muqaddas Mashariki.

Msemaji wa Hamas, Hazim Qassem

Hata hivyo Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala khabithi wa Israel siku ya Alkhamisi alidai kuwa, Tel Aviv haitashirikiana na ICC eti kwa kuwa mahakama hiyo yenye makao yake mjini Hague nchini Uholanzi haina mamlaka ya kufuatilia kesi hiyo. Mwanzoni mwa mwezi Februari, Mahakama ya Kimataifa ya ICC ilitangaza kuwa, ina haki kamili ya kufuatilia kesi ya jinai za kivita zilizofanywa na Israel huko Palestina.

Netanyahu amedai kuwa, hatua hiyo ya ICC ya kuchunguza jinai za utawala huo dhidi ya Wapalestina eti inaonesha chuki za mahakama hiyo kwa Mayahudi. 

Tags