Apr 11, 2021 07:45 UTC
  • Ndege za kivita za Iraq zashambulia ngome za magaidi wa ISIS nchini Iraq

Ndege za kivita za Iraq zimeshambulia ngome za magaidi wa ISIS au Daesh katika Milima ya Hamrin mkoani Diyala ambapo magaidi kadhaa wameangamizwa

Idara ya Taarifa za Usalama Iraq imesema ndege za kivita aina ya F-16 zimetekeleza oparesheni hiyo mpya dhidi ya magaidi magharibi mwa Milima ya Hamrin katika fremu ya Kamandi ya Pamoja ya Oparesheni baada ya  kupokea taarifa za siri za walipo magaidi.

Taarifa hiyo imesema katika oparesheni hiyo, Jeshi la Iraq limefanikiwa kuharibi kabisa makao makuu ya magaidi na kuwaua vinara kadhaa wa ISIS waliokuwemo.

Magaidi wa Daesh Iraq

Siku ya Jumapili Waziri Mkuu wa Iraq Mustafa al Kazemi alitangaza kuwa kiongozi nambari mbili wa ISIS pamoja na vinara wengine kadhaa wa kundi hilo la kigaidi wameuawa katika oparesheni za hivi karibuni za kukabiliana na magaidi nchini humo.

Mwishoni mwa mwaka 2017, Iraq ilitangaza kuangamiza kundi la kigaidi la ISIS nchini humo lakini mabaki ya magaidi hao bado wako katika baadhi ya sehemu za nchi hiyo na hutekeleza mashambulizi ya mara kwa mara katika maeneo mbali mbali ya nchi hiyo.

Tags