Apr 11, 2021 12:43 UTC
  • Marekani yasisitiza Israel ni mshirika wake wa kistratejia katika eneo

Waziri wa Ulinzi wa Marekani amesema, utawala wa Kizayuni wa Israel ni mshirika wa kistratejia wa nchi hiyo katika eneo la Asia Magharibi.

Jenerali Lloyd Austin ambaye ametembelea ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu, ameyasema hayo katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari aliofanya na waziri mwenzake wa utawala haramu wa Israel Beny Gantz na kusisitiza kuwa, mashirikiano kati ya Marekani na Israel yana faida kwa uthabiti wa eneo.

Austin amesema, wamefanya mazungumzo juu ya namna kudhamini na kuihakikishia Israel usalama wa muda mrefu na kuiunga mkono katika mchakato wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na nchi za Kiarabu na akaongeza kwamba, serikali ya Rais Joe Biden wa Marekani imejifunga na suala kulinda usalama wa Israel.

Jenerali Lloyd Austin

Waziri wa Vita wa utawala haramu wa Kizayuni wa Israel Beny Gantz amesema, Israel inaitambua Marekani kuwa ni mshirika wake mkuu katika kukabiliana na Iran na akaeleza kwamba, Tel Aviv itaendelea kuwa na ushrikiano wa karibu na Washington ili kuhakikisha kuwa endapo yatafikiwa makubaliano mapya na Iran, hakutatokea mashindano hatari ya silaha katika eneo.

Mwaka 2018, katika kipindi cha urais wa Donald Trump, Marekani ilichukua hatua ya upande mmoja na ya kinyume cha sheria ya kujitoa katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na kuiwekea vikwazo vikali Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, hata hivyo mfuatizi wa Trump, Joe Biden ameonyesha muelekeo wa kuirejesha Washington kwenye makubaliano hayo. Pamoja na hayo, serikali ya Biden hadi sasa haijachukua hatua yoyote ya kivitendo kuhusiana na kurejea kwenye JCPOA.

Msimamo wa rais huyo wa Marekani kuhusiana na kurejea kwenye makubaliano hayo ya nyuklia umewatia wasiwasi viongozi wa utawala wa Kizayuni wa Israel.../

Tags