Apr 11, 2021 13:44 UTC
  • Waziri wa Saudia: Mabaki ya chakula yenye thamani ya riyali bilioni 40 yanamwagwa kila mwaka

Waziri wa mazingira, maji na kilimo wa Saudi Arabia Abdurahman al Fadhli amefichua kuwa, tani milioni nne na 66,000 za mabaki ya chakula zinamwagwa nchini humo kila mwaka, ambazo thamani yake inakadiriwa kuwa ni sawa na riyali bilioni 40 za nchi hiyo.

Ahmad al Fars, mkuu wa shirika la umma la nafaka la Saudia naye pia ameeleza katika taarifa kwamba, kiwango cha mabaki ya chakula kinachomwagwa nchini humo kila mwaka kinagharimu riyali bilioni 40; na suala hilo linaonyesha kuwa, tani milioni nne na 66,000 za chakula zinapotea nchini humo, ambapo wastani wa dunia nzima ni zaidi ya tani bilioni 1.3.

Al Fars ametilia mkazo udharura wa kuongezwa kiwango cha uelimishaji na utoaji fikra na ushauri ili kupunguza upoteaji na umwagaji wa chakula nchini Saudi Arabia na akasema, wanasubiri kupata maoni juu ya tajiriba na hatua zinazochukuliwa na watu katika maisha ya kila siku ili kuepusha umwagaji na upoteaji wa chakula.

Dhifa za israfu

Mnamo mwaka uliopita wa 2020, shirika moja la usalama wa chakula nchini Saudia lilitangaza kuwa, umwagaji wa chakula unaofanywa nchini humo unagharimu zaidi ya riyali bilioni 400 kila mwaka ambazo ni sawa na dola bilioni 106.

Tovuti ya Uingereza ya Economist ilitoa ripoti mwaka 2019 kuhusu kiwango cha umwagaji chakula unaofanywa katika nchi 25 duniani ambazo zinachangia asilimia 87 ya pato ghafi la uzalishaji la dunia nzima na kueleza kwamba, takwimu za utafiti uliofanywa juu ya suala hilo zinaonyesha kuwa, Saudi Arabia inaongoza kwa umwagaji wa kiwango kikubwa zaidi cha chakula duniani…/