Apr 12, 2021 02:46 UTC
  • Al Houthi: Mtoto mmoja wa Yemen anaaga dunia kila sekunde 5 kutokana na athari mbaya za mzingiro wa Saudia

Mkuu wa Kamati Kuu ya Mapinduzi ya Yemen amesema kuwa mtoto mmoja wa Yemen hufariki dunia kila baada ya sekunde 5 kutokana na mzingiro wa kidhalimu wa Saudi Arabia na washirika wake dhidi ya nchi hiyo.

Muhammad Ali al Houthi amesema kuwa, mauaji ya watoto wadogo wa Yemen yanaakisi ugaidi wa nchi na makundi yanayopigana vita dhidi ya taifa hilo ambayo yamevuka mistari yote myekundu na kukanyaga kwa makusudi sheria na hati ya Umoja wa Mataifa.

Al Houthi ameongeza kuwa, siku hizi jumuiya za kimataifa, badala ya kuzilaani nchi mahasimu wa taifa la Yemen kama Marekani, Uingereza, Saudi Arabia na Imarati zinazowaua raia wa Yemen na kulizingira taifa hilo, zinazishukuru nchi hizo wakati zinapofanya jambo dogo sana kama kwa mfano kuruhusu meli kutia nanga katika bandari za Yemen.

Mwezi Machi 2015, Saudi Arabia ikiungwa mkono na Marekani, Imarati na nchi zingine kadhaa iliivamia kijeshi Yemen na kuiwekea mzingiro nchi hiyo wa nchi kavu, baharini na angani ambao unaendelea hadi sasa.

Wizara ya Haki za Binadamu ya Yemen imetangaza kuwa raia 43,582 wameuliwa moja kwa moja na majeshi ya muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia tangu muungano huo ulipoanzisha hujuma za kijeshi dhidi ya nchi hiyo.

Watoto waliouawa na Saudi Arabia wa Yemen

Ripoti iliyotolewa Alkhamisi na wizara hiyo imeeleza kuwa, maelfu ya mashambulio ya kijeshi yaliyofanywa na muungano vamizi wa kijeshi wa Saudia yamesababisha vifo vya watu 43,582 wakiwemo watoto 7,999 na wanawake 5,184. Idadi ya waliopoteza maisha kwa njia isiyo ya moja kwa moja kutokana na vita hivyo ni kubwa zaidi. Kwa mujibu  Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA),  vita vya Saudi Arabia dhidi ya Yemen vimepelekea zaidi ya watu 233,000 kupoteza maisha katika kipindi cha miaka sita iliyopita.