Apr 13, 2021 02:52 UTC
  • Waungaji mkono wa nje wa Hariri ndio chanzo cha kushindwa kwake kuunda serikali ya Lebanon

Licha ya kupita miezi 6 tokea bunge la Lebanon limpigie kura ya kuwa na imani naye, Saad Hariri ameshindwa kuunda serikali mpya na kwa sasa masuala ya nchi hiyo yanasimamiwa na serikali ya muda inayoongozwa na Hassan Diab.

Kuna sababu tofauti zinazotolewa kuhusiana na Saad Hariri, Waziri Mkuu wa Lebanon, kushindwa kuunda serikali mpya ya nchi hiyo, lakini ni wazi kuwa moja ya sababu kuu zinazomzuia kufanikiwa katika uwanja huo, kabla ya jambo lolote jingine zikiwemo tofauti za ndani ya nchi, ni uingiliaji wa moja kwa moja wa waungaji mkono wake wa kigeni.

Saudi Arabia na Imarati kati ya nchi za Kiarabu, Ufaransa kati ya nchi za Ulaya na Marekani ni waungaji mkono wakuu wa nje wa Saad Hariri. Wachezaji hao wa kigeni wanaona kwamba maslahi yao nchini Lebanon yanadhaminiwa tu kwa kutengwa au kudhoofishwa nafasi ya chama cha Hizbullah katika masuala ya nchi hiyo. Hata kama utawala haramu wa Israel hauingilii moja kwa moja masuala ya Lebanon, lakini unataka kuona serikali ya nchi hiyo ikibuniwa kwa ushiriki wa chini kabisa wa Hizbullah na waungaji mkono wake.

Saad Hariri akiwa na mmoja wa waungaji mkono wake wakuu, Saudia

Kwa hakika kile kinachoendelea huko Lebanon ni mashindano makubwa katika upeo wa eneo la Asia Magharibi (Mashariki ya Kati). Mashindano ambayo yamekuwa yakiendelea kwa muda wa miaka sita kati ya mirengo ya mapatano na mapambano, na hasa tokea uingie madarakani utawala wa Mfalme Salman huko Saudi Arabia, yamebadilika na kuwa ugomvi wa wazi kati ya pande hizo. Hizbullah ya Lebanon imekuwa na nafasi muhimu katika kupamana na makundi ya kigaidi na kulinda mfumo wa kisiasa nchini Syria katika hali ambayo Saudi Aabia, Imarati, Ufaransa, Marekani na utawala wa Kizayuni zimekuwa zikishirikiana kwa karibu na serikali ya Uturuki kwa lengo la kuiangusha serikali halali ya Rais Bashar al-Asad wa Syria. Kushindwa ugaidi Syria na kulindwa mfumo wa kisiasa wa nchi hiyo na vile vile kushindwa magaidi wa Daesh katika nchi jirani ya Iraq, kumaimarisha pakubwa nafasi ya mrengo wa mapambano katika eneo.

Ni kwa mtazamo huo ndipo maadui wa Hizbullah wakaanzisha juhudi kubwa za kulidhoofisha kundi hilo la mapambano ya Kiislamu na kutaka kulitoa katika muundo wa madaraka ya Lebanon. Katika uchaguzi wa 2018 maadui hao walitumia pesa nyingi pamoja na vyombo vyao vya habari kwa shabaha ya kuunga mkono mrengo wa Magharibi unaoongozwa na Saad Hariri dhidi ya muungano wa Hizbullah, lakini pamoja na hayo Hizbullah ilifanikiwa kuwashinda maadui wake hao na kwa mara ya kwanza kabisa katika historia ya Lebanon ikaibuka na ushindi wa moja kwa moja wa wingi wa viti bungeni kwa kupata viti 68 kati ya viti vyote 128 vya bunge hilo.

Baada ya kushindwa huko, maadui walianza kutekeleza njama mpya dhidi ya muungano wa kisiasa wa Hizbullah ambapo licha ya kupata ushindi wa moja kwa moja lakini uliwekewa vizingiti ili kuuondoa kabisa au kuudhoofisha katika mfumo wa madaraka ya Lebanon. Juhudi za kisiasa za Hariri za kuunda serikali bila ya ushiriki mkubwa wa Hizbullah ambazo ziliibua ghasia za mitaani Oktoba 2019 na ambazo hatimaye zilimpelekea Hariri kujiuzulu, ghasia zilizozuka kufuatia mlipuko wa bandari ya Beirut na kumpelekea Hassan Diab ajiuzulu nafasi ya uwaziri mkuu na hivi sasa mashinikizo yanayotolewa na Hariri kwa ajili ya kuitenga Hizbullah katika kubuni serikali mpya ya Lebanon ni sehemu ya njama hiyo.

Hassan Diab

Kushindwa Hariri kuunda serikali ya aina hiyo hakujakuwa na matunda mengine isipokuwa kuzidishwa mashinikizo ya kisiasa dhidi yake. Kwa mtazamo huo, tovuti ya Lebanon ya an-Nashra imechapisha ripoti kwa kutegemea vyanzo vya kuaminika vya nchi hiyo kwamba Saudi Arabia ambayo imekuwa katika mstari wa mbele wa waungaji mkono wakuu wa Saad Hariri sasa imegeuka na kuwa miongoni mwa wapinzani wa uwaziri mkuu wake. Kwa msingi huo Hariri ana wasi wasi kwamba iwapo atatangaza serikali yake mpya katika mazingira ya sasa huenda jambo hilo likazua milipuko ya migogoro kadhaa. Hivyo ameamua kusubiri hadi pale mambo yatakapokuwa kwa manufaa yake katika ngazi za kieneo na kimataifa.

Nukta ya kuzingatiwa ni kuwa uingiliaji wa wachezaji wa kigeni katika masuala ya ndani ya Lebanon ni mkubwa kiasi kwamba gazeti la nchi hiyo la al-Akhbar liliandika Jumamosi kuwa: Hassan Diab, Waziri Mkuu anayeseimamia masual ya Lebanon alikuwa amepangikiwa kusafiri Iraq tarehe 17 mwezi huu wa Aprili lakini serikali ya Baghdad inayoongozwa na Mustafa al-Kadhimi ilishinikizwa na wachezaji hao wa kigeni hadi ikasalimu amri na kuamua kufutilia mbali safari hiyo.

Tags