Apr 14, 2021 11:29 UTC
  • Wapalestina wakasirishwa na kitendo chha Wazayuni cha kuzuia adhana kwa kutumia vipaza sauti

Serikali ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina na Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS zimelaani vikali hatua ya utawala haramu wa Israel ya kukata nyaya za vipaza sauti katika Msikiti wa al-Aqswa na kuzuia kuadhiniwa kwa kutumia vipaza sauti.

Nabil Abu Rudeina, msemaji wa Serikali ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina ameitaka jamii ya kimataifa kuchukua hatua za kuzuia vitendo vya kihujuma vya utawala dhalimu wa Israel huko Palestina.

Afisa huyo wa Serikali ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina amesema kuwa, hatua hiyo ya Israel hasa katika kipindi hiki cha mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani ni ya kibaguzi na iliyo dhidi ya matukufu ya kidini na uhuru wa kuabudu kama ambavyo inakiuka wazi hati za kimataifa za haki za binadamu.

Katika miongo ya karibuni, utawala ghasibu wa Kizayuni wa Israel umechukua hatua nyingi kwa lengo la kuubadilisha utambulisho wa Kiislamu wa Quds tukufu, mojawapo ikiwa ni sheria ya kupiga marufuku kusomwa adhana kwa kutumia vipaza sauti katika misikiti ya mji huo.

 

Desemba 23, 2016 Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio 2334 ambalo liliutaka utawala haramu wa Israel usimamishe haraka na kikamilifu shughuli zote za ujenzi wa vitongoji katika ardhi za Palestina unazozikalia kwa mabavu.

Utawala wa Kizayuni ambao unaungwa mkono kikamilifu na Marekani katika hatua zake hizo haramu umedhamiria kubadilisha muundo wa kijiografia na kidemografia wa maeneo ya Palestina; ili kwa kuyazayunisha maeneo hayo, kuhakikisha unazihodhi na kuzidhibiti kikamilifu ardhi za Wapalestina.

Tags