Apr 15, 2021 13:02 UTC
  • Harakati ya Nujabaa: Kuendelea kuwepo kijeshi Marekani ndio hatari kubwa zaidi kwa Iraq

Naibu Katibu Mkuu wa harakati ya muqawama wa Kiislamu ya Nujabaa nchini Iraq amesisitiza kuwa, kuendelea kuwepo kijeshi Marekani, ndio hatari kubwa zaidi inayotishia usalama wa Iraq.

Nasr Ash-Shamri, Naibu Katibu Mkuu wa harakati ya muqawama wa Kiislamu ya Nujabaa ameyasema hayo leo katika ujumbe aliotuma kwa jeshi ghasibu la kigaidi la Marekani akilihutubu: "kutambua na kufikiria namna ya kukabiliana na hatari, ni jukumu la wananchi wote wa Iraq, ambao kila mara wamekuwa wakitaka kukomeshwa ukaliaji wenu ardhi wa kijinai na kuhitimishwa uingiliaji wa kituo chenu cha ujasusi."

Ash-Shamri ameongezea kwa kusema: "leo Marekani, ambayo imepuuza makusudi mpango uliopitishwa na bunge la Iraq kuhusiana na kuondoka askari wa Kimarekani, inaendesha hujuma za angani na ardhini dhidi ya nchi hii, wakati Iraq ni nchi huru na mwanachama wa Umoja wa Mataifa."

Naibu Katibu Mkuu wa harakati ya muqawama wa Kiislamu ya Nujabaa ametoa indhari pia kwa serikali ya Iraq kuhusu matokeo mabaya na hasi ya kuendelea kuwepo kijeshi Marekani, kwa muundo wa kijamii, kiuchumi na kisiasa wa Iraq.

Wananchi wengi pamoja na makundi ya kisiasa ya Iraq wanataka askari wa jeshi la kigaidi  la Marekani waondoke katika ardhi ya Iraq, huku bunge la Iraq, nalo pia likiwa limepitisha mpango kuhusiana na kuondoka askari hao katika ardhi ya nchi hiyo.../

Tags