Apr 16, 2021 03:33 UTC
  • Ansarullah yajibu mapigo baada ya Saudia kuua watoto wa Yemen kwa mabomu

Wanaharakati wa Ansarullah wakishirikiana na vikosi vya jeshi la Yemen wameshambulia kwa makombora na ndege zisizo na rubani (droni) kituo cha mafuta cha Aramco cha Saudi Arabia, siku moja baada ya muungano vamizi unaoongozwa na Riyadh kushambulia kwa mabomu mkoa wa Sa'ada wa kaskazini magharibi mwa Yemen.

Msemaji wa Jeshi la Yemen, Brigedia Jenerali Yahya Saree amesema vikosi vya Yemen mapema jana vilitumia makombora saba ya Sa’ir na Badr pamoja na droni nne za Samad-3 na Qasef-2K katika operesheni dhidi ya kituo hicho cha mafuta cha Saudia pamoja na maeneo mengine nyeti ya utawala huo wa kifalme katika eneo la Jizan, kusini mashariki mwa Saudia.

Amesema moto mkubwa ulitokea katika kituo cha mafuta cha Aramco kufuatia operesheni hiyo, na kwamba makombora na droni za Wayemen zililenga shabaha kwa usahihi mkubwa na kuusababishia hasara kubwa utawala wa Riyadh.

Brigedia Jenerali Saree amesema operesheni ya jana ni jibu kwa ukatili wa muungano vamizi wa Saudia ambao unaendelea kumwaga damu za Wayemen hata katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani.

Kituo cha mafuta cha Aramco cha Saudia kikiteketea

Siku ya Jumatano, ndege za kivita za Saudia zilishambulia kwa mabomu makazi ya raia katika wilaya ya Monabeh, mkoani Sa'ada ulioko kaskazini magharibi mwa Yemen, ambapo watoto wawili waliuawa, huku watu wengine wanne wakijeruhiwa.

Wiki iliyopita, Wizara ya Haki za Binadamu ya Yemen ilitangaza kuwa raia 43,582 wameuliwa moja kwa moja na majeshi ya muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia tangu muungano huo ulipoanzisha hujuma za kijeshi dhidi ya nchi hiyo maskini Machi 2015.

 

 

Tags