Apr 16, 2021 07:43 UTC
  • Mjumbe wa UN: Suluhisho la mgogoro wa Yemen ni la kisiasa

Martin Griffiths, Mjumbe Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoj wa Mataifa katika masuala ya Yemen amesisitiza kuwa, mgogoro wa Yemen unapaswa kutafutiwa suluhisho la kisiasa.

Akizungumza Alhamisi, Griffiths ametaka mgogoro wa Yemen utatuliwe kisiasa huku akisema kuwa, janga la COVID-19 limepelekea matatuzo ya Wayemen yaongezeke maradufu. Amesema Wayemen wanakumbwa na masaibu ya muda mrefu kutokana na vita nchini humo.

Aidha akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Heiko Maas Jumatatu, Martin Griffiths alisema Wayemen wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula na dawa.

Mwezi Machi 2015, Saudi Arabia ikiungwa mkono na Marekani, UAE na nchi zingine kadhaa iliivamia kijeshi Yemen na kuiwekea mzingiro nchi hiyo wa nchi kavu, baharini na angani ambao unaendelea hadi sasa.

Vita hivyo vya Saudia vimesababisha maafa makubwa zaidi ya kibinadamu nchini Yemen.

Watoto ni waathirika wakuu wa vita vya muungano vamizi wa Saudia dhidi ya Yemen

Kwa mujibu  Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA), vita vya Saudi Arabia dhidi ya Yemen vimepelekea zaidi ya watu 233,000 kupoteza maisha katika kipindi cha miaka sita iliyopita. Idadi kubwa ya raia hasa wanawake na watoto ni waathirika wakuu wa hujuma za Saudia dhidi ya Yemen.

Hivi karibuni, Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) lilisema kati ya Januari na Juni 2021, asilimia 54 ya Wayemen, yaani watu milioni 16.2, watakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula kutokana na vita vya Saudia dhidi ya nchi hiyo.