Apr 16, 2021 07:46 UTC
  • Ndege za kivita za Israel zashambulia Ukanda wa Ghaza

Ndege za kivita za utawala haramu wa Israel zimetekeleza mashambulizi dhidi ya eneo la Ukanda wa Ghaza mapema leo asubuhi.

Kwa mujibu wa duru za Palestina, ndege hizo za kivita za Israel zimedondosha mabomu katika eneo la kaskazini mwa Ukadna wa Ghaza. Aidha taarifa zaidi zinasema jeshi la Israel limevurumisha makombora katika eneo la Hjar al Dik katika Ukanda wa Ghaza.

Utawala wa Kizayuni wa Israel umedai kuwa mashambulizi hayo ni jibu kwa maroketi yaliyovurumishwa kutoka Ghaza na kulenga ardhi zinazokaliwa kwa mabavu.

Ndege za kivita, helikopta, droni na vifaru  vya utawala wa Kizayuni katika miezi ya karibuni zimefanya hujuma kwa mara kadhaa katika Ukanda wa Ghaza. 

Mtoto Mpalestina aliyeuawa shahidi katika hujuma za Israel dhidi ya Ghaza

Malefu ya Wapalestina wasio na hatia wameuawa na kujeruhiwa katika mashambulizi ya Israel dhidi ya Ghaza.

Eneo la Ukanda wa Ghaza liko chini ya mzingiro wa anga, nchi kavu na baharini wa Israel tangu mwaka 2006 na hivyo kuwasababishia matatizo na masaibu mengi wakazi wa Kipalestina wa eneo hilo.