Apr 16, 2021 08:02 UTC
  • Kujaribiwa irada na nguvu ya Iran; kosa la kistratijia la Netanyahu

Kumetokea mvutano kati ya utawala haramu wa Israel na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kufuatia hatua ya utawala huo ya kufanya uharibifu katika kutuo cha urutubishaji urani cha Iran katika eneo la Natanz, uharibifu ambao umetajwa na Iran kuwa ni ugaidi wa kinyuklia.

Tarehe 6 Aprili, vibaraka wa Israel walilenga kwa gruneti meli ya Iran ya Saviz ikiwa katika maji ya Bahari ya Sham na siku 6 baadaye yaani tarehe 12 Aprili, kituo cha nyuklia cha Iran kikalengwa na uharibifu wa Israel. Kuna nukta tatu muhimu zinazopasa kuzingatiwa katika matukio hayo ya kigaidi ya Israel dhidi ya maslahi ya Iran.

Nukta ya kwanza ni kuwa Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel hamwamini hata waziri wake wa vita, Benny Gantz, kwa sababu hakumfahamisha uamuzi wake wa kufanya uharibifu huo katika kituo cha nyuklia cha Iran. Akizungumza siku ya Jumanne mwishoni mwa safari ya waziri mwenzake wa Marekani Lloyd Austin, katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na utawala ghasibu wa Israel, Benny Gantz amesema kwamba ameomba uchunguzi ufanyika haraka katika mashirika ya ujasusi ya utawala huo ya Mosad na Shin Bet kuhusu uharibifu huo katika kituo cha Natanz. Gantz amesema kuwa ni jambo baya na hatari kwa kiongozi wa utawala huo kutowajibika na kuchukua hatua za kibinafsi na kisiasa ambazo zinahatarisha usalama wa Wazayuni. Matamshi hayo yanathibitisha wazi kwamba mvutano wa kisiasa kati ya viongozi wa utawala huo umewapelekea wasiweza kufanya mashauriano ya lazima kati yao, hata yale yanayohusu usalama wa utawala huo.

Benny Gantz

Nukta ya pili ni kwamba uharibifu huo umefanyika katika hali ambayo duru mpya ya mazungumzo kati ya Iran na kundi la 4+1 yanaendelea huko Vienna Austria na ripoti zinazotolewa zinaoonyesha kuwa pande mbili hizo zimeridhishwa na hatua iliyopigwa katika mazungumzo hayo. Netanyahu ambaye katika utawala wa Donald Trump nchini Marekani alifanya juhudi kubwa hadi kumshawishi kiongozi huyo aiondoe Marekani katika mapatano ya nyuklia ya IAEA, hivi sasa hana matumaini makubwa na serikali mpya ya Marekani inayoongozwa na Rais Joe Biden, na kwa msingi huo ameamua kufanya uharibifu katika kituo cha nyuklia cha Natanz ili kuvuruga mazungumzo ya Vienna.

Katika makala iliyoandikwa na Yonah Jeremy Bob, mwandishi anayejihusisha na masuala ya usalama, ujasusi na ugaidi katika gazeti la Kizayuni la Jerusalem Post ameandika kwamba licha ya kutojulikana vyema wakati ambao Marekani inapasa kurejea katika mapatano ya JCPOA, lakini ni wazi kwamba utawala wa Kizayuni umeamua kufanya uharibifu katika kituo cha nyuklia cha Natanz ili kuvuruga mazungumzo yanayoendelea mjini Vienna.

Utawala wa Tel Aviv umeamua kufanya ujaribifu katika kituo cha urutubishaji madini ya urani huko Natanz katika hali ambayo mivutano ya kisiasa imepamba moto huko Isreal na katika upande wa pili kuna uwezekano wa kupigwa hatua nzuri katika mazungumzo ya Iran na nchi za Magharibi mjini Vienna. Gazeti la Jerusalem Post limeutaja uharibifu huo wa Israel kuwa vita vyake vya siri dhidi ya Iran jambo ambalo Benny Gantz ametahadharisha vikali juu yake.

Nukta ya tatu ni kuwa inaonekana kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa sasa imeweka pembeni siasa zake za 'subira ya kistratijia' kuhusiana na hatua hizo za uharibifu wa Israel na kuamua kulipiza kisasi dhidi ya utawala huo wa kigaidi. Iran inaamini fika kwamba hatua hizo za uharibifu hazijatekelezwa bila ya ufahamu kamili wa Marekani na hata baadhi ya nchi za Ulaya. Hivyo katika hatua ya kwanza ya radiamali yake, Iran imeamua kuuongeza kiwango cha urutubisha madini ya urani hadi asilimia 60. Kuhusu hilo, Ali Akbar Salehi, Mkuu wa Taasisi ya Nishati ya Atomiki ya Iran anasisitiza kwamba hatua hiyo ya Iran imechukuliwa katika kivuli cha sheria ya hatua ya kistratijia iliyopasishwa karibuni na Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge) kwa ajili ya kuondoa vikwazo vya kidhalimu dhidi ya taifa la Iran. Kwa ibara nyingine ni kwamba hatua za uharibifu za Israel dhidi ya maslahi ya Iran si tu hazitadhoofisha nguvu ya nyuklia ya Iran bali zitachangia na kuimarisha zaidi azma ya Tehran ya kuchukua hatua muhimu zaidi katika mapatano ya JCPOA.

Mashinepewa za kurutubisha urani zilizotengenezwa na wataalamu wa ndani ya Iran

Maudhui ya mwisho ni kuwa, kufikia sasa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imefanya juhudi kubwa kwa ajili ya kuzuia kuibuka vita vipya katika eneo la Asia Magharibi (mashariki ya Kati), lakini kwa kuitilia maanani uwezo wake mkubwa wa kiulinzi (Iran), kuendelea hatua za uchochezi na uharibifu za Israel huenda kukalisukuma eneo hili katika vita vipya, jambo ambalo viongozi wengi na hata wa ndani ya Israel yenyewe, wamekuwa wakitahadharisha juu yake. Huenda Netanyahu anajaribu kuibua vita vipya katika eneo kwa lengo la kujikwamua katika hali ngumu ya kisiasa aliyomo ndani yake kwa sasa huko Israel bila ya kujali usalama wa utawala huo wa Kizayuni, lakini ni wazi kuwa iwapo vita  vitazuka, bila shaka hatima ya uhai wa utawala huo wa kigaidi haitakuwa tena mikononi mwake.