Apr 16, 2021 12:04 UTC
  • Wapalestina 4,500 wanashikiliwa katika korokoro za utawala ghasibu wa Israel

Jumuiya ya Mateka wa Kipalestina imetangaza kuwa, Wapalestina 4,500 wakiwemo wanawake 41 na watoto 140 wanaendelea kushikiliwa katika mahabusu za utawala wa Kizayuni wa Israel.

Ripoti iliyotolewa leo Ijumaa na taasisi kadhaa za Kipalestina kwa mnasaba wa Siku ya Mateka ikiwemo Jumuiya ya Mateka wa Kipalestina na Kituo cha Kutetea Uhuru na Haki za Kiraia imesema kuwa, mateka wa Kipalestina wanaoshikiliwa katika jela na korokoro za Israel wanaendelea kusumbuliwa na ukiukaji mkubwa wa sheri za kimataifa katika jela hizo.

Ripoti hiyo imeongeza kuwa, Wazayuni wa Israel wamezidisha ukiukaji wa sheria za kimataifa na sasa wanatumia ugonjwa wa corona kama silaha mpya inayotumika kuwatesa na kuwanyanyasa wafungwa wa Kipalestina. 

Awali Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) ilikuwa imetangaza kuwa, tangu mwaka 1967 hadi sasa mateka wasiopungua 220 wa Kipalestina wameuawa shahidi katika jela za Israel. 

Mateka wa Kipalestina wananyanyaswa

Mateka na wafungwa wa Kipalestina wanaoshikiliwa katika jela za Israel wamekuwa wakisumbuliwa na sulubu na mateso ya kutisha katika jela za Israel.

Hivi karibuni, Idara ya Habari inayohusika na masuala ya mateka Wapalestina ilitangaza kuwa, Waziri wa Usalama wa Ndani wa utawala wa Kizayuni ameagiza mateka Wapalestina wa masuala ya usalama wasipigwe chanjo ya corona na kwamba chanjo hiyo itolewe kwa wafanyakazi tu wa magereza wanakoshikiliwa Wapalestina hao, uamuzi ambao unahalifu taratibu na hati za kimataifa.

Tags