Apr 18, 2021 06:28 UTC
  • Viongozi wa UAE wamtumia salamu za pongezi Rais Assad kwa mnasaba wa siku ya uhuru wa Syria

Kiongozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), naibu wake na mrithi wa ufalme wa Abu Dhabi, wamemtumia, kwa nyakati tofauti, Rais Bashar al Assad wa Syria salamu za pongezi kwa mnasaba wa kuadhimisha siku ya uhuru na kufikia tamati kukaliwa kwa mabavu nchi hiyo na Wakoloni Wafaransa.

Kiongozi wa Imarati (UAE) Khalifa bin Zayd Al Nahyan, Muhammad bin Rashid Al Maktoum, waziri mkuu na naibu Kiongozi wa umoja huo wa falme za Kiarabu pamoja na Mohammad bin Zayd Aal Nahyan, mrithi wa ufalme wa Abu Dhabi na Kaimu Kamanda Mkuu wa vikosi vya ulinzi vya Imarati, kila mmoja amemtumia ujumbe Rais Bashr al Assad kumpa salamu za pongezi kwa mnasaba wa Siku ya Taifa ya Syria.

Hivi karibuni, Imarati imechukua hatua kadhaa kwa madhumuni ya kufufua uhusiano wake na Syria sambamba na harakati ambazo nchi mbali mbali za Kiarabu zinaonyesha kwa ajili ya kuirejesha Syria kwenye Jumuiya ya Nchi za Kiarabu.

Siku Syria ilipopata uhuru

Kabla ya salamu za viongozi wa Imarati, Rais wa Syria alipokea pia salamu za pongezi kwa mnasaba wa Siku ya Taifa ya nchi hiyo kutoka kwa marais na viongozi wa Iran, Russia, Malaysia pamoja na Kiongozi wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina.

Mnamo tarehe 17 Aprili kila mwaka, wananchi wa Syria husherehekea siku wakoloni Wafaransa walipoondoka katika ardhi ya nchi yao. Kuondoka askari wa mwisho wa Ufaransa katika ardhi ya Syria tarehe 17 Aprili 1946, ndiko kulikopelekea siku hiyo kuitwa Siku ya Uhuru wa Syria.../

Tags