Apr 21, 2021 09:37 UTC
  • Bernie Sanders
    Bernie Sanders

Seneta wa kujitegemea wa Marekani, Bernie Sanders ameitaka serikali ya nchi hiyo kubana misaada yake kwa utawala wa Kizayuni wa Israel kwa shabaha ya kuushinikiza ukomeshe kukalia kwa mabavu ardhi ya Palestina.

 Bernie Sanders ambaye alikuwa akihutubia mkutano wa kila mwaka wa lobi ya Mayahudi ya J Street ameashiria msaada mkubwa wa kijeshi wa Marekani kwa Israel na kusema: Ukweli ni kwamba, wananchi wa Marekani hawataki kuona fedha zao zikitumiwa kuunga mkono siasa zinazokiuka haki za binadamu na mienendo inayowatambua raia wa Palestina kuwa ni watu wa daraja la pili. Sanders ametoa wito wa kuwepo udharura wa kuishinikiza ipasavyo Israel ikiwa ni pamoja na kubana na kupunguza misaada ya Marekani kwa utawala huo, kwa sababu ya mienendo ya Tel Aviv inayoharibu fursa za kurejesha amani.

Katika miaka ua karibuni seneta huyo mashuhuri wa Marekani mwenye asili ya Kiyahudi amekuwa akikosoa vikali misaada na himaya isiyo na mpaka ya Washington kwa serikali ya Tel Aviv na amemtaja mara kadhaa Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu kuwa ni mbaguzi. 

 Kwa upande wake seneta wa chama cha Democratic, Elizabeth Warren ameuambia mkutano wa J Street kwamba: "Kama tunataka kusitisha ujenzi wa vitongoji vya walowezi na kusaidia pande zote kufikia mapatano ya kuunda nchi mbili basi hatuna budi kutumia nyenzo zote zinazowezekana, la sivyo hatutakuwa tumewajibika." 

Elizabeth Warren

Kila mwaka serikali ya Marekani huipatia Israel mabilioni ya dola za walipakodi katika sura ya misaada ya kijeshi na kiuchumi. Misaada hiyo na mikataba ya kijeshi ya Marekani na Israel imekuwa ikiibua maandamano ya upinzani karibu kila mwaka katika maeneo mbalimbali ya Marekani. Waandamanaji hao wanasema, fedha za walipakodi wa Marekani zinatumiwa katika hujuma na ukatili wa utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya raia wa Palestina. 

Wakati huo huo ukosoaji huyo wa wazi wa seneta huyo dhidi ya misaada mikubwa ya Washington kwa utawala wa Kizayuni wa Israel na jinai nyingine za utawala huo huko Palestina kwa hakika unafichua mwenendo usio wa kibinadamu wa serikali ya Marekani wa kuiunga mkono kibubusa Israel bila ya kujali jinai na uhalifu wake. Marekani ndiye muungaji mkono na mfadhili mkubwa zaidi wa jinai na uhalifu unaofanywa na Israel dhidi ya watu wa Palestina na misaada mikubwa ya kifedha na silaha inayotolewa na Washington inatumaka katika njia hiyo. Javid Qurban Oughli ambaye ni mchambuzi wa masuala ya Asia Magharibi anasema: Katika siasa za nje za Marekani kuna msingi wa kistratijia na unaoheshimiwa na vyama vyote ambao nguzo yake kuu ni kuwa na muungano wa kistratijia na Israel. Kwa mujibu wa msingi huo, ambao ni mwongozo wa mienendo ya kisiasa na kiusalama ya serikali ya Washington, Marekani inaahidi kulinda uwepo wa Israel na usalama wake na kuisaidia katika nyanja mbalimbali.

Trump na Netanyahu

Serikali ya Marekani daima inatilia mkazo suala la kuendelezwa misaada na himaya kubwa ya kijeshi na kiuchumi kwa utawala wa Kizayuni wa Israel kwa kadiri kwamba, katika kipindi cha utawala wa Barack Obama, serikali ya Washington ilipasisha kifurushi cha misaada ya kijeshi cha miaka kumi kwa Tel Aviv. Hata hivyo Donald Trump alikwenda mbali zaidi na kuzidisha misaada hiyo kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa. Trump alithubitu kufanya mambo ambayo hata marais wa kabla yake wa Marekani walijizuia kuyafanya. Trump pia alibariki ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi iliyoghusubiwa mwaka 1967 ya Palestina na alikuwa akiunga mkono na kutetea mauaji yanayofanywa na utawala ghasibu wa Israel dhidi ya raia wasio na hatia wa Palestina kwa kisingizio eti cha kujilinda.

Inatupasa kusema kuwa, kama si misaada ya kifedha ya Marekani inayofikia dola bilioni 4 kwa mwaka, basi Israel haitakuwa tena na uwezo wa kuwakandamiza Wapalestina wana kuendeleza ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni au kuzishambulia nchi mbalimbali.           

Tags