Apr 22, 2021 03:46 UTC
  • Mlipuko mkubwa katika kiwanda nyeti cha makombora cha Israel

Mlipuko mkubwa umejiri katika kiwanda nyeti cha utawala wa Kizayuni wa Israel ambacho hutumika kutengeneza makombora.

Kwa mujibu wa taarifa, mlipuko huo ulijiri Jumanne katika 'majaribio ya kawaida' ya silaha za kisasa.

Hakuna taarifa zilizotolewa kuhusu kupoteza maisha watu waliokuwa katika eneo hilo.

Duru za Kizayuni zinadokeza kuwa kiwanda hicho kinachojulikana kama Tomer hutengeneza makombora na injini za maroketi.

Wakaazi wa eneo hilo wanasema walisikia mlipuko mkubwa na kisha wakaona wingu kubwa linalofanana na uyoga juu ya kiwanda hicho, ambacho kiko katika mji wa Ramla na ambacho huzalisha maroketi na makombora ambayo hutumiwa na jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel.

Kombora la Arrow 4 ambalo lilikuwa likiundwa katika kiwanda cha Israel kilichoshuhudia mlipuko mkubwa

Kiwanda hicho kilianzishwa mwaka 2018 na kinafungamana na wizara ya vita ya Israel na hutumika pia kuunda aina mpya ya makombora ya kisasa ya balistiki ya Arrow-4

Mwezi Februari waziri wa vita wa Israel Benny Gantz alijigamba kuwa kombora hilo la Arrow-4 linaundwa kwa ushirikiano na Marekani na kwamba litakuwa na teknolojia ya kiwango cha juu kwa ajili ya vita vya baadaye katika eneo la Asia Magharibi.

 

Tags