Apr 23, 2021 10:08 UTC
  • ‘Quds’, mhimili mkuu katika uchaguzi wa Bunge la Palestina

Utawala wa Kizayuni wa Israel unajaribu kuvuruga mchakato wa uchaguzi wa Bunge la Palestina katika mji wa Quds (Jerusalem) hatua ambayo imekabiliwa na tahadhari kutoka kwa makundi ya kupigania ukombozi wa Palestina.

Uchaguzi wa  Bunge la Palestina unatazamiwa kufanyika katika kipindi cha siku 20 zijazo katika Ukingo wa Magharibi, Quds inayokaliwa kwa mabavu na Ukanda wa Ghaza. Huu utakuwa uchaguzi wa kwanza kufanyika tangu miaka 14 iliyopita kwa lengo la kuwachagua wabunge Wapalestina. Utawala haramu wa Israel unaishinikiza Mamlaka ya Ndani ya Palestina iakhirishe uchaguzi ili ufanyike wakati mwingine.

Kuna sababu mbili muhimu ambazo zimepelekea Israel  itake kuzuia kufanyika uchaguzi wa bunge la Palestina wakati huu. Kwanza ni kuwa, Israel ina wasi wasi mkubwa kuwa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, itapata ushindi na kuunda serikali ambayo mhimili wake utakuwa ni muqawama na mapambano.

Sababu ya pili ni kuwa Israel inataka kuzuia uchaguzi kufanyika katika mji wa Quds. Hii ni kwa sababu Israel inafahamu kuwa Wapalestina hawakubali hata kidogo hatua ya Quds kufanywa kuwa mji mkuu wa utawala wa Israel. Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump mnamo Disemba 2017 alichukua uamuzi ulio kinyume cha sheria na kutangaza kutambua Quds kuwa mji mkuu wa Israel na mwaka 2018 akatangaza kuuhamishia ubalozi wa Marekani katika mji huo unaokaliwa kwa mabavu.

Pamoja na hayo, mbali na Wapalestina, nchi nyingi duniani hazitambui Quds kuwa mji mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel na hivyo wakuu wa Israel wanapinga uchaguzi wa bunge la Palestina kufanyika katika mji wa Quds ambao wanaotazama kama sehemu ya ardhi za Palestina wanazozikali kwa mabavu.

Nabil Abu Rudeineh

Kwa msingi huo Israel inatumia mbinu mbali mbali kuzuia kufanyika uchaguzi wa bunge la Palestina mjini Quds ili kadiri muda unavyosonga mble nchi nyingi zaidi zihamishie balozi zao mjini humo.

Sera hii ya Israel imekabiliwa na upinzani mkali na onyo kutoka kwa makundi ya kupigania ukombozi wa Palestina. Wapalestina wanasisitiza kuwa Quds ni sehemu isiyotenganika ya ardhi ya Palestina na hivyo wana azma ya kufanya uchaguzi katika mji huo. Nabil Abu Rudeineh, Msemaji wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina siku ya Alhamisi alisisitiza kuwa, uchaguzi wa bunge la Palestina utafanyika katika muda ulioainishwa. Aidha amesema Quds ni mstari mwekundu wa Wapalestina na kwamba taifa la Palestina katu halitalegeza msimamo kuhusu mji huo na hawataridhika na mipaka ya muda.

Uchaguzi wa sasa ni fursa kwa Wapalestina kuufanya uamuzi wa Trump wa kutangaza Quds kuwa mji mkuu wa Israel usiwe na maana.

Pamoja na hayo iwapo kwa sababu yoyote ile Wapalestina watabatilisha uamuzi wa kufanya uchaguzi Quds, hatua kama hiyo itamaanisha wameuacha mji wa Quds utawaliwe kikamilifu na Israel.

Hivyo Wapalestina wanafahamu vyema taathira ya kutofanyika uchaguzi wa bunge mjini Quds na wameutahadharisha utawala wa Kizayuni wa Israel kuhusu njama zake za kuvuruga uchaguzi huo.

Wapalestina wakibainisha chuki zao kwa Trump na Netanyahu

Tahadhari hiyo haijatolewa tu na makundi ya muqawama bali hata makundi mengine ya kisiasa ya Palestina pia yamesisitiza kuhusu kufanyika uchaguzi katika mji wa Quds na wameutahadharisha utawala wa Kizayuni kuhusu suala hilo. Kwa msingi huo Mundhar al Haik mwanachama mwandamizi wa Harakati ya Fath ya Palestina amesema kumeanzishwa mapambano ya kuhakikisha utawala wa Israel hauzuii uchaguzi kufanyika katika Quds. Amesema hakuna uchaguzi utakaofanyika Palestina iwapo Quds pia haitahusishwa.

Naye Mohammad Al Ghul mwanachama wa Kamati Kuu ya Harakati ya Wananchi Kwa Ajili ya Ukombozi wa Palestina pia amesisitiza kuhusu mshikamano wa kitaifa katika kukabiliana na njama za Israel kuzuia uchaguzi ufanyike katika mji wa Quds. Amesema sasa kumeanza Intifadha mpya na kubwa ya kuhakikisha uchaguzi hauakhirishwi. Aidha amesema kutofanyika uchaguzi mjini Quds ni jambo lisilokubalika na kuongeza kuwa, utawala wa Kizayuni unalenga kuutenganisha mji huo na maeneo mengine ya Palestina.

Kwa upande wake Taysir Khalid, mwanachama wa kamati ya utendaji katika Harakati ya Ukombozi wa Palestina, PLO,  amesema kuakhirishwa uchaguzi kutazidisha hitilafu na mambo yatavurigika kitaifa Palestina jambo ambalo litapelekea raia wengi wapoteze matumaini.

 

Tags