Apr 23, 2021 12:00 UTC
  • Haaretz: Chokochoko za Netanyahu dhidi ya Iran ni sawa na kucheza na moto

Gazeti la Kizayuni la Haaretz limemtahadharisha Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel likieleza kuwa, chokochoko za Benjamin Netanyahu dhidi ya Iran ni sawa na kucheza na moto na kwamba zinaweza kuwa na matokeo mabaya kwa Israel.

Haaretz limeandika katika moja ya makala zake kwamba, baada ya meli ya Iran kushambuliwa katika Bahari Nyekundu na uharibifu uliofanyika katika taasisi ya kurutubisha madini ya Urani ya Natanz, Israel inapaswa kuwa imesahafahamu kuwa, inapaswa kuacha kumimina mafuta ya petroli katika moto.

Gazeti la Haaretz limeashiria ahadi ya Iran ya kulipiza kisasi kwa matukio hayo mawili dhidi yake na kueleza kwamba, Israel inapaswa kuipa uzito kauli hiyo ya Iran hasa kwa kuzingatia tajiriba ya huko nyuma.

Tarehe 6 mwezi huu wa Aprili, meli ya kibiashara ya Saviz ya Iran iiharibiwa baadhi ya sehemu zake baada ya kutokea mlipuko katika Bahari Nyekundu jirani na pwani ya Djibouti.

Aidha Jumapili ya wiki iliyopita, sehemu moja ya umeme ya taasisi ya urutubishaji urani ya Shahid Ahmadi Roushan katika kituo cha nyuklia cha Natanz ilikumbwa na hitilafu.

Kituo cha nyuklia cha Natanz

 

Viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wamesema kuwa, utawala haramu wa Israel ndio uliohusika na tukio na wametangaza kuwa, kisasi cha chokochoko hiyo kitalipwa wakati na eneo mwafaka.

Utawala wa Kizayuni wa Israel ulijigamba kuwa ndio uliofanya uharibifu huo huku vyombo vya habari vya Magharibi vikilivalia njuga mno suala hilo mpaka kufikia kudai kuwa eti urutubishaji urani nchini Iran utasimama kwa miezi kadhaa kutokana na uharibifu huo.

Hata hivyo kazi ya urutubishaji urani kwa asilimia 60 inaendelea katika kituo hicho na matunda yake yameanza kutolewa.

Tags