May 04, 2021 11:04 UTC
  • Madai ya Rais Biden ya kudhoofika al-Qaeda na kukabiliana na ugaidi

Rais Joe Biden wa Marekani Jumapili iliyopita alidai sambamba na kuanza kuondoka askari wa Marekani nchini Afghanistan baada ya miongono miwili kwamba, Washington itaendelea kufuatilia nyendo za magaidi na kusambaratisha aina yoyote ile ya tishio la ugaidi nchini Afghanistan.

Biden alisema kuwa, ‘’tutaendelea kuwa macho katika pembe zote za duniani kuhusiana na suala la makundi ya kigaidi.”

Rais wa Marekani sanjari na kuashiria kutimia miaka 10 tangu kuuawa Osama bin Laden aliyekuwa kiongozi wa kundi la mtandao wa al-Qaeda amesema kuwa: Kundi la kigaidi la mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda limedhoofika mno huko nchini Afghanistan na kwamba, Marekani imetekeleza ahadi zake za kulisaka kundi la al-Qaeda na viongozi wake huko nchini Afghanistan.

Biden amesisitiza kuwa, Marekani haitaacha kutekeleza ahadi yake ya kuzuia kukaririwa matukio kama la Septemba 11. Matamshi ya Biden kuhusiana na kudhoofika mtandao wa al-Qaeda na vilevile sisitizo lake kukabiliana na ugaidi a ameyatoa bila ya kuashiria hata kwa mbali nafasi na mchango wa Marekani katika kuundwa kundi hilo la kigaidi na vilevile  kuenea ugaidi wa kitakfiri katika eneo la Asia Magharibi.

Askari wa Marekani nchini Afghanistan

 

Katika kipindi cha vita baridi Marekani ilikuwa na mchango katika kuundika kundi la mtandao wa al-Qaeda baada ya kukaliwa kwa mabavu Afghanistan na dola la Urusi ya zamani. Ukweli wa mambo ni kuwa, Marekani ikiutumia ugaidi kama wenzo, ilikuwa muungaji mkono mkubwa wa makundi ya kigaidi na yenye kuchupa mipaka ukiwemo mtandao wa al-Qaeda.

Katika kipindi cha Afghanistan kukaliwa kwa mabavu na Umoja wa Kisovieti katika muongo wa 80 ikiwa na lengo la kukabiliana na kuenea fikra za ukomunisti, ilichukua hatua ya kuwapatia silaha maelfu ya watu waliokuwa wametoka katika maeneo mbalimbali ya dunia na kwenda Afghanistan kwa ajili ya kupigana na vikosi vya Urusi. Huu ndio uliokuwa mwanzo wa kuenea harakati za kigaidi wa al-Qaeda kwa uongozi wa Osama bin Laden.

Baadaye yaani katika muongo wa 90 Osama bin Laden sambamba na kuukosoa utawala wa Aal Saud kutokana na kuweko vikosi vya Marekani katika nchi hiyo ikiwa eneo lenye maeneo mawili matakatifu ya Waislamu alianzisha kile alichokiita kuwa jihadi dhidi ya ukafiri wa Kimarekani kwa kushambulia maeneo mbalimbali yenye maslahi na Marekani zikiwemo balozi za Washington huko Dar es Salaam Tanzania na Nairobi Kenya.

Wanamgambo wa Taliban

 

Hatimaye kundi la mtandao wa al-Qaeda Septemba 11 mwaka 2001 likafanya hujuma na mashambulio katika miji ya New York na Washington. Kuanzia mwaka 2011 na kuendelea Marekani ikiwa na lengo la kuiangusha serikali ya Syria na kudhoofisha mhimili wa muqawama ilianza kuyaunga mkono makundi ya kitakfiri likiwemo tawi la al-Qaeda katika nchi hiyo ya Kiarabu yaani Jabhat al-Nusra.

Kundi hili la kigaidi ambalo hivi sasa linafanya harakati zake katika mkoa wa Idlib nchini Syria kwa anuani ya Hay'at Tahrir al-Sham hadi sasa lingali linaungwa mkono na madola ya Magharibi na kuanzia wakati huo, limekuwa likitumiwa kama wenzo wa kuishinikiza serikali ya Damascus.

Jambo jingine ambalo limezungumziwa na Joe Biden ni Marekani kufungamana na suala la kukabiliana na ugadi nchini Afghanistan na maeneo mengine ya dunia na kadhalika kuzuia kutokea tena tukio kama la Septemba 11.

Madai haya yanaweza kutathmini kama ni majibu kwa wale wanaopinga kuondoka askari wa Marekani nchini Afghanistan hususan katika Kongresi ya nchi hiyo na kuwapa hakikisho kwamba, Washinghton itaendelea kufuatilia nyendo za makundi ya kigaidi nchini Afghanistan na katika meneo mengine ya dunia. Hivi karibuni Biden alitangaza uamuzi wa kuviondoa vikosi vya Marekani nchini Afghanistan na akasisitiza kuwa, zama za kufikia tamati vita vya muda mrefu kabisa vinavyoishughulisha Washington sasa umewadia.

Zalmay Khalizad, mjumbe maalumu wa Marekani katika masuala ya Afghanistan amedai kuwa, kuendelea kubakia majeshi ya Washington nchini Afghanistan si kwa maslahi ya ikulu ya White House.

Zalmay Khalizad, mjumbe maalumu wa Marekani katika masuala ya Afghanistan

 

Kwa muktadha huo, kuondoka askari wa Marekani kabla ya kuwa ni hatua iliyochukuliwa katika fremu ya mpango ulioratibiwa na wenye upeo wa mbali katika uga wa kupambana na ugaidi nchini Afghanistan na katika maeneo mengine ya dunia, inaonyesha kugonga mwamba Marekani na kutokuwa na natija yoyote ya maana ya uwepo wa kimabavu wa askari wake katika nchi hiyo kwa muda wa miongo miwili na kushindwa kuusambaratisha ugaidi kinyume na ilivyodai wakati inaivamia nchi hiyo.

Fauka ya hayo, madai haya ya Rais Biden kuhusiana na kuendelea kupambana na ugaidi nchini Afghanistan yamepokewa kwa shaka kubwa. Frank Gardner, mwandishi wa habari wa masuala ya usalama anasema: Askari wa Marekani, Uingereza na Shirika la Kijeshi la NATO wanaondoka nchini Afghanitan katika msimu huu wa joto tulionao.

Hii ni katika hali ambayo, wapiganaji wa kundi la wanamgambo wa Taliban wamekuwa wakipata nguvu siku baada ya siku huku makundi ya kigaidi ya al-Qaeda na Daesh yakiwa yameshadidisha hujuma na mashambulio yao. Ukweli wa mambo ni kuwa, katika mustakabali kuyasambaratisha makundi ya kigaidi ya al-Qaeda na Daesh litakuwa jambo gumu zaidi hasa katika maeneo ya mbali na yanayofikiwa kwa shida nchini Afghanistan.

Tags