May 08, 2021 08:06 UTC
  • Saudia yaua raia Wayemen waliokuwa  wakielekea katika maandamano ya Siku ya Quds

Raia wasiopungua saba wameuawa nchini Yemen katika mkoa wa Majzar baada ya ndege za kivita za muungano vamizi wa Saudia kushamabulia raia waliokuwa wanajitayarisha kushiriki katika maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds jana Ijumaa.

Taarifa zinasema hujuma hiyo imetekelezwa dhidi ya wakazi wa kijiji cha Sahari katika mkoa wa Majzar ambapo mbali na raia hao kuuwa wengine kadhaa wamejeruhiwa.

Shirika rasmi la habari la Yemen, Saba, limesema ndege za kivita za muungano vamizi wa Saudia zilidondosha mabomu wakati wanakijiji walikuwa wanajitayarisha kuandaa maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds ya kuunga mkono Wapalestina na kulaani jinai za utawala haramu wa Israel.

Hujuma hiyo ya Saudia ya kuwalenga raia wa Yemen waliokuwa wanapanga kushiriki katika maandamano ya Siku ya Quds imelaaniwa vikali na imetajwa kuwa thibitisho la wazi kuwa, ufalme wa Saudia una utambulisho wa Kizayuni.

Watoto wa Yemen ni waathirika wakuu wa uvamizi wa Saudia

Tarehe 26 Machi 2015, Saudi Arabia kwa msaada wa Marekani, utawala wa Kizayuni wa Israel, Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) na baadhi ya nchi za Ulaya na Kiarabu kama Uingereza na Sudan, ilianzisha mashambulizi ya kivamizi ya pande zote dhidi ya taifa maskini la Kiarabu na Kiislamu la Yemen. Muungano huo wa Saudia pia umekuwa ukishirikiana kwa karibu na makundi ya kigaidi katika vita vyake hivyo dhidi ya Yemen.

Wavamizi hao walikuwa na ndoto ya kuvimaliza vita hivyo katika kipindi cha wiki chache tu. Hata hivyo huu ni mwaka wa 7 na kadiri siku zinavyopita, ndivyo wananchi wa Yemen wanavyozidi kuwa imara katika muqawama na kujihami kwao kishujaa.