May 09, 2021 05:50 UTC
  • Hatimae Arab League yajitutumua kujadili jinai za utawala wa Kizayuni

Hatimaye Jumuiya ya nchi za Kiarabu (Arab League) imeamua kuitisha kikao cha kuchukua maamuzi kuhusu jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel kufuatia ombi la Mamlaka ya Ndani ya Palestina.

Kwa mujibu wa shirika la habri la FARS, jana Arab League ilitangaza kuwa kesho Jumatatu itaitisha kikao cha dharura cha kuchukua maamuzi kuhusu njia za kukabiliana na jinai za israel huko Quds, baada ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina kuwasilisha ombi rasmi la kuitishwa kikao hicho.

Kabla ya hapo, Riyadh al Maliki, Waziri wa Mambo ya Nje wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina alitaka kuitishwe vikao vya dharura vya taasisi na vyombo mbalimbali vya kimataifa kwa shabaha ya kuwaunga mkono Wapalestina mbele ya jinai za Wazayuni.

Riyadh al Maliki, Waziri wa Mambo ya Nje wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina

 

Riyadh al Maliki alisema amewasiliana na mabalozi wa Palestina nje ya nchi katika mkakati wa kuitishwa mikutano ya dharura ya kimataifa ya Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC), Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama la umoja huo.

Al Maliki aliongeza kuwa, Mamlaka ya Ndani ya Palestina inafanya jitihada za kuhakikisha kwamba, mikutano ya jumuiya hizo inatoa taarifa zinazolaani jinai na uhalifu unaondelea kufanywa na Israel na kuzihimiza nchi mbalimbali zikate uhusiano wao na utawala huo wa ubaguzi wa rangi kwa sababu ya kutenda jinai dhidi ya binadamu.

Katika siku za karibuni utawala ghasibu wa Israel umezidisha hujuma na mashambulizi yake ya kinyama dhidi ya Wapalestina wa Quds inayokaliwa kwa mabavu. Shirika la Hilali Nyekundu La Palestina limetangaza kuwa, Wapalestina wasiopungua 208 walijeruhiwa Ijumaa ya wiki hii pekee katika hujuma na mashambulizi ya wanajeshi wa Israel dhidi ya Wapalestina huko Quds wakiwemo wale waliokuwa katikati ya Sala ndani ya Msikiti wa al Aqsa.

Tags