May 09, 2021 12:38 UTC
  • Instagram yatoa tamko baada ya kufunga akaunti za waungaji mkono wa Palestina

Mtandao wa kijamii wa Instagram umelazimika kutoa tamko kufuatia malalamiko ya maelfu ya watumiaji wa mitandao ya kijamii kutokana na kufungwa akaunti za watu walioonyesha uungaji mkono wao kwa Wapalestina wakazi wa eneo la Sheikh Jarrah Baitul Muqaddas (Jerusalem) inayokaliwa kwa mabavu.

Katika ujumbe kwa watumiaji wake, mtandao wa kijamii wa Instagram umeeleza kusikitishwa na kile ulichoeleza kuwa ni matatizo yaliyojitokeza kwa sababu ya hitilafu za kiufundi katika mfumo mzima wa mtandao huo wa kijamii na kuahidi kuwa matatizo hayo yatatatuliwa haraka.

Katika ujumbe huo Instagram imedai kuwa, matatizo ya kiufundi yaliyojitokeza katika siku kadhaa za hivi karibuni na kusababisha kuzuka masuala mbali mbali kuhusiana na jumbe zinazohusu matukio tofauti yaliyojiri duniani, zikiwemo za matukio muhimu kama yale ya karibuni huko Sheikh Jarrah, sambamba na Siku ya Kimataifa ya Quds, yote hayo yamesababishwa na hitilafu za kiufundi katika mfumo mzima wa mtandao huo wa kijamii.

Hujuma za askari wa Kizayuni katika msikiti wa Al Aqsa

Sambamba na maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Quds na katika hatua ya kuunga mkono utawala haramu wa Kizayuni wa Israel, mitandao ya kijamii, ikiwemo ya Twitter na Instagram ilizifunga akaunti za makumi ya watu kwa sababu ya kutoa mwito wa kutangazwa mshikamano na wakazi wa eneo la Sheikh Jarrah, huko Quds tukufu inayokaliwa kwa mabavu na kuakisi jinai zinazofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari, akaunti hizo katika mtandao wa Twitter zilifungwa kwa sababu ya kusambaza ujumbe kwa lugha za Kiarabu na Kingereza usemao "Iokoeni Sheikh Jarrah".../