May 10, 2021 07:49 UTC
  • Mataifa ya Kiafrika yalaani uvamizi wa Wazayuni dhidi ya Masjidul-Aqswa

Mataifa ya Kiislamu barani Afrika yametoa taarifa ya kulaani hujuma na uvamizi wa jeshi la utawala haramu wa Israel dhidi ya Msikiti wa al-Aqswa, kibla cha kwanza cha Waislamu.

Mataifa hayo sambamba na kulaani hujuma na mashambulio ya jeshi la utawala haramu wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina na Msikiti wa al-Aqswa yamezitaka asasi na jumuiya za kimataifa kutekeleza majukumu yao kwa kuliunga mkono taifa madhulumu la Palestina.

Sehemu nyingine ya taarifa hiyo imeeleza kuwa: Hujuma na uvamizi wa jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Masjidul-Aqswa unakinzana wazi kabisa na sheria za kimataifa pamoja na haki za binadamu.

Katika siku za karibuni utawala ghasibu wa Israel umezidisha hujuma na mashambulizi yake ya kinyama dhidi ya Wapalestina wa Quds inayokaliwa kwa mabavu.

Mpalestina akisaidiwa baada ya kujeruhiwa kufuatia uvamizi wa Wazayuni huko Baitul-Muqaddas

 

Wapalestina wasiopungua 208 walijeruhiwa Ijumaa iliyopita iliyosadifiana na maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Quds katika hujuma na mashambulizi ya wanajeshi wa Israel dhidi ya Wapalestina huko Quds na katika kitongoji cha Sheikh Jarrah. 

Tangu ulipoanza mwezi mtukufu wa Ramadhani mwaka huu, Wapalestina wa mji wa Baitul-Muqaddas wameshuhudia kuongezeka hujuma na mashambulio dhidi yao yanayofanywa na wanajeshi wa Israel na hivyo kukwamisha harakati zao za kidini na kiibada katika mwezi huu tukufu.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linatazamiwa kuitisha kikao leo ili kuzungumzia matukio yanayoendelea kujiri katika mji wa Baitul-Muqaddas unaokaliwa kwa mabavu na eneo la Sheikh Jarrah katika mji huo.

Tags