May 11, 2021 12:16 UTC
  • Wanamuqawama wa Palestina wafanya shambulio kubwa sana la maroketi dhidi ya vitongoji vya Wazayuni

Duru za Palestina zimeripoti kuwa wanamapambano wa makundi ya muqawama wamefanya mashambulio makubwa ya maroketi dhidi ya vitongoji ya walowezi wa Kizayuni vya Ashdod na Asghalan kaskazini ya Ukanda wa Gaza.

Hayo yamethibitishwa pia na redio ya jeshi la utawala haramu wa Kizayuni wa Israel ambayo imeripoti leo kuwa, hadi sasa Waisraeli 31 wamejeruhiwa katika kitongoji cha Asghalan na kukimbizwa kwenye kituo cha tiba cha Barzilaye.

Brigedi za Izzuddin al Qassam, tawi la kijeshi ya Harakati ya Muqawama Kiislamu ya Palestina HAMAS zimeeleza katika taarifa kwamba, zimefanya shambulio kubwa la makombora dhidi ya vitongoji vya Ashdod na Asghalan katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu, kujibu hatua ya adui ya kuzishambulia nyumba na vikosi vya wanamuqawama wa Palestina na kutoa onyo kwa utawala wa Kizayuni kwamba, mashambulio yajayo yatakuwa makubwa zaidi.

Picha zilizotolewa na duru za Kizayuni zinaonyesha jengo moja lililoshambuliwa kwa maroketi kadhaa ya wanamuqawama wa Palestina.

Hujuma za Israel Ukanda wa Gaza

Wakati huo huo waziri mkuu wa utawala haramu wa Israel Benjamin Netanyahu, amefanya kikao cha dharura na maafisa wa usalama na kijeshi wa utawala huo wa Kizayuni, ambacho kimehudhuriwa pia na waziri wa vita Benny Gantz, mkuu majeshi Aviv Kochavi na mshauri wa usalama wa ndani Meir Ben Shabbat.

Katika upande mwingine, ndege za kivita za utawala wa Kizayuni zimeshambulia maeneo kadhaa mashariki ya Ukanda wa Gaza na jengo moja la ghorofa nane la makazi ya watu magharibi mwa eneo hilo, ambapo kwa mujibu wa wizaya ya afya ya Palestina, Wapalestina 24 wameuwa shahidi na wengine 103 wamejeruhiwa katika mashambulio hayo.

Kufuatia jinai za kinyama zinazoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina, Rais Mahmoud Abbas wa Mamlaka ya Ndani amefuta sherehe maalum za kuadhimisha Idul-Fitri na kuamuru bendera za Palestina zipeperushwe nusu mlingoti.../