May 11, 2021 14:17 UTC
  • Kikao kisicho na tija cha Baraza la Usalama kuhusu Quds sanjari na ukwamishaji mambo wa Marekani

Kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusiana na hali ya mambo huko Quds Palestina kilifanyika Jumatatu ya jana tarehe 10 Mei na kumalizika bila ya natija yoyote.

Wanadiplomasia walioko katika Umoja wa Mataifa wanasema kuwa, kikao cha Baraza la Usalama kuhusu matukio ya Quds kilimalizika bila ya kufikiwa natija ya kutolewa taarifa ya pamoja katika hali ambayo, Marekani haikuona kama ni jambo linalofaa kwa wakati huu kutolewa taarifa jumla kuhusiana na matukio ya huko Quds.

Marekani iliwataka na kuwasisitizia washirika wake kwamba, hivi sasa kunapaswa kufanyika juhudi za nyuma ya pazia za kutuliza hali ya mambo na kwamba, haina uhakika kama kutolewa taarifa wakati huu litakuwa jambo zuri na linalofaa.

Imeamuliwa kuwa, wanachama wa Baraza la Usalama waendelee na mazungumzo kwa ajili ya kuandaa taarifa yenye kemeo laini na isiyo na lugha kali kwa pendekezo la Norway kwa nchi 15 wanachama wa baraza hilo. Muswada wa azimio hilo ulioandaliwa kwa pamoja baina ya Tunisia na China unautaka utawala haramu wa Israel usimamishe shughuli zake za ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni na uache kubomoa nyumba za Wapalestina na kuwafukuza kutoka katika maeneo yao likiwemo eneo la Quds Mashariki.

Uvamizi wa wanajeshi wa Israel huko Baitul-Muqaddas

 

Aidha taarifa hiyo inataka kuweko na hali ya kujizuia na kuheshimu hali ya sasa ya maeneo matakatifu. Kadhalika muswada huo unaelezea wasiwasi mkubwa ulionao kuhusu mzozo na vitendo vya utumiaji mabavu vinavyoongezeka katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan likiwemo eneo la Quds Mashariki, mahala ambapo hivi karibuni pameshuhudia mamia ya watu wakijeruhiwa.

Licha ya wasiwasi wa kidhahiri uliooneshwa na serikali ya Rais Joe Biden wa Marekani kuhusiana na hali ya sasa huko Quds Mashariki, lakini misimamo ya Washington katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na hatua yake ya kuzuia kutolewa hata taarifa ambayo haina kemeo kali na ambayo haikosoi sana hatua za utawala wa Kizayuni huko Quds Mashariki inaonyesha kuwa, Marekani haiko tayari kuvumilia hata ukosoji mdogo kabisa kuhusiana na utendaji wa kijinai wa Israel dhidi ya Wapalestina.

Swali ambalo linaulizwa hivi sasa ni ni hili kwamba, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ikiwa nguzo kuu muhimu ya asasi hii ya kimataifa ambayo ina jukumu la kulinda amani na usalama wa dunia, hivi kwa mtazamo wa Marekani asasi hii ina jukumu la kushughulia hali mbaya na maafa wanayokabiliwa nayo Wapalestina hususan wa Quds Mashariki na vilevile mashambulio mapya ya kinyama ya Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza au taasisi hii ya kimataifa inapaswa kunyamaza kimya na kutochukua hatua yoyote kama vile hakuna kilichotokea?

 

 

Tukitupia jicho misimamo ya Marekani katika Baraza la Usalama kuhusiana na kufuatiliwa hatua za Israel iwe ni dhidi ya Wapalestina au dhidi ya nchi jirani kama Syria na Lebanon tunaona kuwa, hakuna wakati ambao serikali ya Washington hususan katika kipindi cha utawala wa Donald Trump ambapo iliruhusu kupasishwa azimio linalokosoa utendaji wa Israel.

Ni mara moja katika kipindi cha utawala wa Barack Obama mwaka 2016 ambapo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipasisha azimio nambari 2334 likiitaka Israel isitishe ujenzi wa vitongoji vyake vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Palestina zilizokaliwa kwa mabavu mwaka 1967. Marekani ilijizuia kupiga kura katika mchakato wa kupigiwa kura azimio hilo ambalo liliitaja hatua hiyo ya Israel kuwa ni ukiukaji wa sheria za kimataifa.

Katika kipindi cha utawala wa Rais Trump, Marekani ilitekeleza siasa za kutoa himaya na uungaji mkono wa pande zote kwa utawala haramu wa Israel ambapo mwaka 2018, Washington iliamua kujitoa katika Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa ikilalamikia kukosolewa utawal huo ghasibu.

Javid Qurban Oghlo, mtaalamu wa masuala ya Asia Magharibi anasema: Katika sera za kigeni za Marekani, kuna msingi mkuu wa kistratejia na usiozingatia mrengo wa vyama ambao umejengekeza juu ya kuwa na umoja wa kistratejia na Israel.

Mpalestina akisaidiwa baada ya kujeruhiwa kufuatia uvamizi wa Wazayuni huko Baitul-Muqaddas

 

Hii ni katika hali ambayo, utawala haramu wa Israel unahesabiwa kuwa mkiukaji mkuu wa haki za binadamu ulimwenguni. Mbali na kufanya mauaji dhidi ya Wapalestina hususan katika Ukanda wa Gaza, kuwafukuza Wapalestina kutoka katika makazi yao katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Quds Mashariki na kughusubu ardhi zao, Israel imekuwa ikijenga kwa kasi vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika maeneo ya Wapalestina.

Tukio la karibuni kabisa kuhusiana na suala hilo, ni njama za Wzayuni za kuwafukuza Wapalestina kutoka katika kitongoji cha Sheikh Jarrah huko Quds Mashariki. Hatua hiyo imepelekea Wapalestina wengi kuwa wakimbizi. Bila shaka huo ni ukiukaji wa wazi wa haki za binadamu na ni jinai ya kivita. Pamoja na hayo, serikali ya Biden inayodai kuwa kinara wa haki za binadamu, imepuuza hatua na jinai hizo za utawala ghasibu wa Israel na kuendelea kuunga mkono utawala huo na hivyo kutosheka tu na kutoa tamko la kuonyesha wasiwasi wa kile kinachojiri huko Palestina.

Tags