May 12, 2021 10:31 UTC
  • Israel yakataa pendekezo la UN la kusitisha mashambulizi dhidi ya Wapalestina

Duru za Palestina zimeripoti kuwa, utawala haramu wa Israel umekataa pendekezo la mjumbe wa Umoja wa Mataifa la kusitisha mashambulizi mara moja dhidi ya watu wa Palestina.

Ripoti zinasema Tor Wennesland Mratibu Maalumu wa Umoja wa Mataifa katika Masuala ya Amani ya Mashariki ya Kati ametoa pendekezo la kusitisha mapigano kwa utawala wa Kizayuni wa Israel lakini Tel Aviv imekataa pendekezo hilo. 

Ripoti zinasema kuwa, Wennesland ametahadharisha kuwa, iwapo vita havitasitishwa mapigano ya sasa yatapanuka na kuwa vita kubwa ambayo itakuwa vigumu kuidhibiti. 

Kwa zaidi ya wiki mbili sasa mji wa Quds na Msikiti wa al Aqsa vimeshuhudia mashambulizi ya wanajeshi katili wa utawala wa Kizayuni wa Israel wakiwahujumu Waislamu waliokuwa wakitekeleza ibada ya Swala ndani ya Msikiti wa al Aqsa na raia wengine wa Palestina. Mashambulizi hayo ya kinyama ya Israel yamejibiwa kwa makombora na maroketi ya wanamapambano wa Palestina yaliyovurumishwa dhidi ya miji ya utawala huo haramu ukiwemo mji mkuu, Tel Aviv. 

Mashambulizi ya Israel dhidi ya watu wa Gaza

Taarifa ya Wizara ya Afya ya katika eneo la Ukanda wa Gaza inasema kuwa, raia wasiopungua 43 wa Kipalestina wameuawa shahidi hadi jana katika mashambulizi ya jeshi la Israel na wengine 296 wamejeruhiwa. 13 kati ya mashahidi hao ni watoto wadoto. 

Tags