May 13, 2021 06:29 UTC
  • Wapalestina wakipinga uvamizi wa Israel
    Wapalestina wakipinga uvamizi wa Israel

Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amesema kuwa Quds ni mstari mwekundu na mji mkuu wa milele wa Palestina na amesisitiza uilazima wa kuendelea kutetea haki za taiifa la Palestina kwa kukabiliana na wavamizi wa Kizayuni.

Mahmoud Abbas amesema kuwa, Quds imewaunganisha Wapalestina wote dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel na kwamba hakutapatikana amani, suluhu wala utulivu bila ya Quds kukombolewa kutoka kwenye makucha ya wavamizi.

Abbas ameongeza kuwa: "Raia wa Palestina wametoa neno lao na sisi kama walivyo Wapalestina wote, tunataka mustakbali usio na uvamizi wala ujenzi wa vitongoji vya walowezi katika ardhi ya Palestina.

Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amesema Israel imefanya jinai za kivita na mauaji ya kizazi huko Quds inayokaliwa kwa mabavu na kwamba vijana wanaoilinda Quds wanasimama imara kukabiliana na wavamizi wanaotaka kutwaa nyumba na makazi yao.

Mahmoud Abbas

Machafuko ya sasa katika ardhi za Palestina yalianza baada ya wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel kuvamia na kuvunjia heshima Msikiti wa al Aqsa na raia wa Wapalestina wa mji wa Quds waliokuwa wakifanya ibada ya itikafu katika msikiti huo. Wanajeshi katili wa utawala wa Kizayuni wa Israel wamewahujumu Waislamu waliokuwa wakitekeleza ibada ya Swala ndani ya Msikiti wa al Aqsa na raia wengine wa Palestina. Israel pia imekuwa ikishambulia vikali mji wa Gaza na hadi sasa makumi ya raia wa Palestina wameuawa kwa mshambulizi ya ndege za kivita za utawala huo haramu.

Taarifa ya Wizara ya Afya ya katika eneo la Ukanda wa Gaza inasema kuwa, raia wasiopungua 69 wa Kipalestina wameuawa shahidi hadi jana katika mashambulizi ya jeshi la Israel na wengine 388 wamejeruhiwa. 17 kati ya mashahidi hao ni watoto wadoto na 7 ni wanawake. 

Tags