May 13, 2021 08:10 UTC
  • Yemen yajibu mapigo, yashambulia kampuni ya mafuta ya Aramco na uwanja wa ndege wa Najran, Saudia

Msemaji wa jeshi al Yemen ametangaza kuwa, wapiganaji wa nchi hiyo wamefanya mashambulizi makubwa ya makombora na ndege zisizo na rubani dhidi ya kampuni ya mafuta ya Aramco na uwanja wa ndege wa Najran nchini Saudi Arabia.

Yahya Saree amesema mapema leo kwamba, operesheni hiyo kubwa ya kijeshi imefanyika kwa kutumia makombora 7 ya balestiki aina ya Badr na Sa'ir na ndege 5 zisizo na rubani aina ya Qasef 2k. Msemaji wa jeshi la Yemen ameongeza kuwa, hujuma hiyo imefanyika kujibu mashambulizi ya Saudi Arabia na washirika wake wanaoendelea kuizingira Yemen. 

Jumapili iliyopita pia ndege zisizo na rubani za Yemen zilishambulia kambi ya kijeshi ya Mfalme Khalid katika mkoa wa Asir huko kusini mwa Saudia Arabia. 

Tarehe 26 Machi 2015, Saudi Arabia kwa msaada wa Marekani, utawala wa Kizayuni wa Israel, Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) na baadhi ya nchi za Ulaya na Kiarabu kama Uingereza na Sudan, ilianzisha mashambulizi na uvamizi wa pande zote dhidi ya taifa maskini na la Kiislamu la Yemen. Muungano huo wa Saudia pia umekuwa ukishirikiana kwa karibu na makundi ya kigaidi katika vita vyake hivyo dhidi ya Yemen.

Watoto wa Yemen, wahanga wakuu wa mashambulizi ya Saudia

Maelfu ya Wayemeni wameuawa na mamilioni ya wengine wamelazimika kuwa wakimbizi ndani ya nje ya nchi hiyo kutokana na mashambulizi ya Saudia na washirika wake.