May 13, 2021 08:49 UTC
  • Safari ya  Amir wa Qatar Saudi Arabia

Amir wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad al-Thani, tarehe 10 Mei alifanya safari chini Saudia Arabia ambapo alikutana na kuzungumza na Muhammad bin Salman, Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa nchi hiyo.

Uhusiano wa nchi mbili hizo umepitia misukosuko mingi katika miaka ya karibuni. Mwezi Juni 2017 Saudi Arabia kwa kisingizio cha kulalamikia siasa za kieneo za Qatar ilishirikiana na nchi nyingine tatu za Kiarabu za Imarati, Bahrain na Misri katika kukata uhusiano wa kidiplomasia na nchi hiyo na kuizingira pande zote. Pamoja na hayo lakini Qatar ilisimama imara na kutosalimu amri mbele ya mashinikizo na mzingiro wa nchi hizo. Baada ya Rais Donald Trump wa Marekani, ambaye alikuwa muungaji mkono mkuu wa Muhammad bin Salman katika siasa zake za kieneo, kushindwa katika uchaguzi, hatimaye Saudia ililazimika kulegeza msimamo na mwezi Januari mwaka huu ikaanza kufanya juhudi za kuhuisha uhusiano na Qatar.

Safari ya Sheikh Tamim mjini Riyadh ni ya pili kufanyika katika miezi mitano ya hivi karibuni. Safari yake ya kwanza ilifanyika mjini Riyadh Januari mwaka huu ampapo alishiriki katika kikao rasmi wa watawala wa Saudia na hivyo kuhitimisha mvutano uliokuwepo kati ya pande mbili. Safari ya mara hii imefanyika kutokana na mwaliko rasmi wa Mfalme Salman wa Saudia Arabia ambao uliwasilishwa rasmi kwa Sheikh Tamim na Faisal bin Farhan, Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudia tarehe 28 Aprili.

Mzingiro wa Saudia na washirika wake dhidi ya Qatar

Kinyume na ilivyokuwa safari iliyofanyika mwezi Januari, safari ya mara hii kimsingi imelenga kujadili masuala ya kieneo. Kwa mujibu wa vyanzo vya kuaminika, mazungumzo hayo yamekita katika majadiliano ya Iran na kundi la 4+1, hali ya Yemen na vilevile mgogoro wa Palestina.

Qatar ni moja ya nchi za Kiarabu ambazo zimeamua kuwa na uhusiano mzuri na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na wala haijakubali kutumbukia kwenye mtego wa siasa za uhasama dhidi ya Iran ambazo zinatekelezwa na baadhi ya nchi za Kiarabu zikiongozwa na Saudi Arabia. Katika upande wa pili, Qatar daima imekuwa ikijishughulisha na masuala ya utatuzi wa migogoro inayoendelea katika nchi za eneo. Pamoja na kuwa katika kipindi ambapo uhusiano wa Iran na Saudi Arabia ulikuwa umekatika, uhusiano wa Qatar na nchi hiyo pia ulikuwa umekatwa, lakini hivi sasa Doha inafanya juhudi za kupatanisha nchi mbili hizi. Akizungumza Alhamisi iliyopita, Muhammad bin Abdurrahman Aal Thani, Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar alisema kwamba nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi zinapaswa kushirikiana na Iran na kubuni mfumo mmoja wa kuondoa hofu na kupunguza mivutano ya kieneo.

Saudi Arabia na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita zimekuwa zikionyesha hamu ya kufanya mazungumzo kwa ajili ya kuhuisha uhusiano wa pande mbili. Katika ulegezaji msimamo wa wazi, Muhammad bin Salman, Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudia amesema kwamba nchi yake inataka kuwa na uhusiano mzuri na Iran. Pamoja na hayo lakini kinyume na ilivyo Qatar, Saudia ingali ina dhana mbaya na wasiwasi kuhusu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, wasiwasi ambao kimsingi unatokana na siasa zake za ushindani katika eneo. Ni wazi kuwa katika safari yake ya karibuni mjini Riyadh, Sheikh Tamim amewajulisha watawala wa Saudia msimamo wa Iran kuhusu uhusiano wake na nchi hiyo, masuala ya kieneo na mazungumzo ya mjini Vienna.

Yemen ni suala jingine ambalo limejadiliwa na Qmir wa Qatar na watawala wa Saudia katika safari yake nchini humo. Vita vya kichokozi vya muungano unaoongozwa na Saudia dhidi ya nchi hiyo masikini ya Kiarabu vimeingia katika mwaka wake wa saba na matukio ya medani ya vita nchini humo na hasa katika mkoa wa Ma'rib hayako kwa maslahi ya watawala wa Riyadh. Qatar inataka vita hivyo visimamishwe mara moja. Baada ya kuona kuwa haifiki popote katika hujuma yake dhidi ya watu wa Yemen bali badala yake imekuwa ikabiliwa na mashambulio makali ya jeshi na kamati za wananchi wa Yemen katika ardhi yake yenyewe, watawala hao hatimaye wamekosa budi na hivyo kuamua kuanzisha mazungumzo na Serikali ya Wokovu wa Taifa la Yemen. Kuna uwezekano mkubwa kwamba Qatar ndiyo itakayoandaa mazungumzo hayo.

Sheikh Tamim (kushoto) katika mazungumzo na Mfalme Salman wa Saudia

Suala jingine ni kuwa safari ya Sheikh Tamim nchini Saudia imefanyika sambamba na kufanyika hujuma kali na ya kinyama ya utawala haramu wa Israel dhidi ya Wapalestina katika eneo la Quds Mashariki na Ukanda wa Gaza. Nchi mbili hizo zimelaani mashambulio hayo. Inaonekana nchi hizo zinapanga kuitisha kikao cha Jumuiya ya Nchi ya Kiarabu kwa ajili ya kujadili suala hilo na kuwa wapatanishi kati ya Israel na Wapalestina kwa shabaha ya kumaliza mapigano ya pande mbili.

Nukta ya mwisho ni kwamba Saudia sasa imeamua kurekebisha siasa zake za nje kwa kufuatilia masuala ya kupunguza mivutano kati yake na nchi nyingine za eneo na bila shaka inahitajia suala hilo kwa lengo la kuboresha sura yake iliyoharibika katika eneo kutokana na siasa hizo za hujuma na uchokozi dhidi ya mataifa mengine ya eneo.