May 14, 2021 03:31 UTC
  • Safari ya Zarif mjini Damascus; uungaji mkono wa Iran kwa uchaguzi wa Syria

Muhammad Jawad Zarif Waiziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameonana na kuzungumza mjini Damascus na Rais Bashar Asad wa Syria kuhusu uhusiano wa pande mbili, matukio ya Asia Magharibi na uchaguzi mkuu wa rais wa nchi hiyo.

Jumatano zarif alielezea kuridhishwa kwake na maandalizi ambayo yamefanywa na serikali ya Syria kwa ajili ya kufanikisha uchaguzi huo na kusisitiza kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaunga mkono uchaguzi huo na kutumai kuwa utafanyika kwa njia nzuri na katika mazingira ya kuridhisha.

Safari ya Zarif nchini Syria katika kipindi hiki muhimu ambapo nchi hiyo inajiandaa kufanya uchaguzi wa rais ni ishara tosha na ya wazi kwamba Tehran inaupa umuhimu mkubwa mwenendo mzima wa kisasa wa nchi hiyo na kuheshimu maoni ya wananchi wake. Inaamini kwamba njia pekee ya kutatua matatizo ya Syria ni kupitia maamuzi ya kisiasa na kuheshimiwa matakwa ya wananchi. Kuhusu hilo, Rais Asad amesema safari ya Zarif nchini humo katika kipindi hiki muhimu cha kujiandaa kwa ajili ya uchaguzi mkuu ina umuhimu mkubwa.

Zarif (kushoto) na Rais Bashar al-Asad

Uchaguzi wa rais wa Syria umepangwa kufanyika tarehe 26 mwezi huu ambapo wagombea watatu wanashiriki. Wakati ulipoanza mgogoro wa Syria na nchi za kigeni kushirikiana na makundi sugu ya kigaidi kwa ajili ya kuiondoa madarakani serikali halali ya nchi hiyo, Iran ilipinga vikali suala hilo na kusisitiza kuwa njia pekee ya kutatua mgogoro huo ni kupitia njia ya kisiasa na kuheshimiwa maamuzi ya wananchi. Iran ingali inasisitiza suala hilo na kufanya juhudi za kutatua mgogoro huo kwa msingi wa mapatano ya Astana kwa ushiriki wa Iran, Russia na Uturuki.

Mapatano hayo yanasisitiza juu ya utatuzi wa kisiasa wa mgogoro wa Syria, kuheshimiwa serikali halali ya nchi hiyo, utawala na ardhi yake yote pamoja na kupambana na makundi ya kigaidi. Mapatano hayo yameweza kuudhibiti mgogoro huo na kurejesha nchini utulivu wa kiwango fulani. Kufanyika uchaguzi katika mazingira tulivu ndilo takwa kuu la wananchi wa Syria na sasa hilo linakaribia kutimia kupitia Mapatano ya Astana.

Kabla ya hapo serikali halali ya Syria iliponea chupuchupu kuondolewa madarakani kupitia ghasia, vita vya umwagaji damu na uharibifu wa makundi ya kigaidi, jambo ambalo halikuwa na matokeo mengine isipokuwa mauaji, umwagaji damu na uharibifu mkubwa kwa madhara ya watu wa Syria. Pamoja na hayo lakini mapambano ya watu na jeshi la Syria, yalivunja njama za Marekani na utawala haramu wa Israel ya kutaka kuipindua serikali halali ya Bashar Asad na kubadilisha mkondo wa mambo katika eneo nyeti la Asia Magharibi, na hivyo kuimarisha nguvu na nafasi ya watu wa Syria katika matukio ya eneo.

Katika mazingira hayo ni muhimu kutoa uungaji mkono kwa serikali na watu wa Syria katika kukabiliana na mabaki ya magaidi waliotawanyika katika pembe tofauti za nchi hiyo na ndio maana Muhammad Jawad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran katika mazungumzo yake hapo Jumatano mjini Damascus na Waziri mwenzake wa Mambo ya Nje wa Syria, Faisal Miqdad akasema kwamba Iran inaunga mkono serikali na watu wa Syria katika mapambano yao dhidi ya janga la fikra za kupindukia mipaka na ugaidi.

Zarif (kushoto) akiwa na waziri mwenzake wa Syria, Faisal Miqda

Ni wazi kuwa kuimarisha usalama na kupatikana utulivu wa kudumu nchini Syria kutaimarisha zaidi uhusiano wa Tehran na Damascus. Kufunguliwa balozi ndogo za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika miji ya Halab na Ladhiqiyah huko Syria kunabainisha wazi kuimarika uhusiano na ushirikiano wa kisiasa na kiuchumi wa nchi mbili. Iran na Syria zina uhusiano wa kistratijia na bila shaka uungaji mkono wa Iran kwa serikali halali ya Syria katika mapambano yake dhidi ya makundi ya kigaidi, ulizuia kikamilifu kutekelezwa bidaa hatari ya kupinduliwa serikali halali za mataifa kupitia vita na ugaidi wa kimataifa.

Tags