May 14, 2021 08:20 UTC
  • Jihad Islami: Hatima ya wanajeshi wa Israel itakuwa ni kuuawa au kutekwa wakivamia Ghaza

Harakati ya kupigania ukombozi wa Palestina ya Jihad Islami imesema endapo utawala wa Kizayuni wa Israel iwapo utaanzisha vita vya nchi kavu dhidi ya Ghaza basi askari Wazayuni hawatakuwa na hatima nyingine ghairi ya kuuawa au kutekwa nyara na hivyo hiyo itakuwa njia rahisi zaidi kwa harakati za kupigania ukombozi au muqawama kupata ushindi.

Hayo yamedokezwa na Abu Hamza Msemaji wa Saraya Al Quds, tawi la kijeshi la Jihad Islami ya Palestina ambaye ameongeza kuwa: "Mujahidina wameonyesha hamasa katika kukabiliana na utawala ghasibu  na makundi ya muqawama yanatoa muhanga wanajeshi wake katika medani ya vita." 

Ameongeza kuwa, katika siku hizi za Idul Fitri, wanamapambano wa Palestina wako katika vita au wanauawa shahidi kwa ajili ya kutetea mji wa Quds na Msikiti wa Al Aqsa.

Aidha amesema taifa la Palestina limekumbatia mapambano na kujitolea muhanga na hivyo hatimaye litapata ushindi. Kamanda wa Saraya Al Quds amesema makundi ya muqawama na kupigania ukombozi wa Palestina yataendelea kuwa imara hata kama utawala wa Kizayuni umetekeleza mamia ya mashambulizi ya anga na kusababisha uhairbifu mkubwa. Amesema uvamizi huo wa utawala wa Kizayuni hauwezi kusambaratisha haki ya Wapalestina ya kutetea haki yao. 

Wakati huo huo Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, imesema imelenga vituo vya ngao ya kujihami angani vya utawala wa Kizayuni wa Israel maarufu kama 'Kuba la Chuma"

Askari wa harakati za muqawama Palestina akiwa katika eneo la kuvurumisha makombora yanayolenga Israel

Taarifa ya Brigedi za Ezzedin Qassam Tawi la Kijeshi la Hamas imesema makombora ya Sijjil yalivurumishwa katika kituo cha anga cha Hatzerim ambacho kinatumiwa na ndege za utawala wa Israel ambazo zinadondosha mabomu Ghaza.

Hadi sasa Wapalestina 109, wakiwemo watoto 28, wameuawa shahidi tokea Jumatatu wakati utawala wa Kizayuni wa Israel ulipoanzisha mashambulizi dhidi ya Ghaza huku wengine 580 wakiwa wamejeruhiwa.

Utawala ghasibu wa Israel ulianzisha uvamizi dhidi ya Ghaza baada ya Wapalestina katika eneo hilo kuandamana kulalamikia vikali ukandamizaji wa Israel dhidi ya Wapalestina katika mji wa Quds (Jerusalem). Kitendo cha askari katili wa Israel kuuvamia Msikiti wa Al Aqsa mjini Quds na kuwahujumu Wapalestina waliokuwa wakiswali katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kimehesabiwa kuwa ni kuvuka mstari mwekundu wa Wapalestina na Waislamu duniani.

Katika kujibu jinai hizo za Israel makundi ya kupigania ukombozi wa Palestina katika Ukanda wa Ghaza yamevurumisha mamia ya makombora katika miji ya Israel ukiwemo mji mkuu Tel Aviv na kusababisha hasara kubwa. Waisraeli  wasiopungua 7 wameangamizwa katika oparesheni hizo za ulipizaji kisassi za Wapalestina.