May 15, 2021 04:26 UTC
  • Makumi ya Walebanon wavuka mpaka na kuingia Palestina inayokaliwa kwa mabavu

Vyombo vya habari vimeripoti kuwa makumi ya Walebanon wamevunja uzio wa mpaka wa pamoja wa nchi hiyo na ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu zilizopewa jina la Israel na kuingia katika ardhi hizo kuonyesha uungaji mkono wao kwa wananchi wanaodhulumiwa wa Palestina.

Tovuti ya habari ya Arab48 imeripoti kuwa, Ijumaa jioni makumi ya wananchi wa Lebanon waliandamana hadi kwenye mpaka wa pamoja wa nchi yao na Palestina inayokaliwa kwa mabavu (Israel), ambapo baada ya kuvunja uzio wa mpaka, waliingia kwenye ardhi hizo zinazokaliwa kwa mabavu na kutangaza kuwa, lengo la hatua yao hiyo ni kuwaunga mkono wananchi madhulumu wa Palestina na muqawama wa Quds na Gaza.

Kwa mujbu wa duru hiyo ya habari, askari wa utawala haramu wa Kizayuni wa Israel walifyatua risasi upande walikotokea wananchi hao wa Lebanon sambamba na kutoa tangazo kwa walowezi wa Kizayuni wanaoishi karibu na mpaka wa pamoja na Lebanon kuwataka wasitoke majumbani mwao.

Kabla ya tukio hilo la Ijumaa jioni, duru za habari ziliripoti pia kwamba, maelfu ya Wajordan waliandamana hadi kwenye mpaka wa pamoja wa nchi yao na Palestina inayokaliwa kw mabavu kwa lengo la kuwaunga mkono wananchi na muqawama wa Palestina. Wananchi hao wa Jordan waliwataka viongozi wao wafungue mipaka ili waweze kwenda kuwasaidia wananchi wa Palestina.

Ismail Haniya

Hatua hiyo imekuja baada ya Ismail Haniya, Mkuu wa ofisi ya kisiasa ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS kuyatolea mwito mataifa yote ya Kiarabu na Kiislamu pamoja na watetezi wa haki duniani kote wajitokeze kuunga mkono msikiti wa Al Aqsa na Ukanda wa Gaza na kutoa msukumo kwa wananchi wa Palestina.

Tokea ulipoanza mwezi mtukufu wa Ramdhani hadi sasa, mji wa Baitul Muqaddas (Jerusalem) unaokaliwa kwa mabavu na baadhi ya miji mingine ya Palestina inashuhudia makabiliano kati ya askari wa utawala haramu wa Israel na waandamanaji na waumini Wapalestina wanaopinga mwendelezo wa jinai na njama za uyahudishaji zinazofanywa na utawala wa Kizayuni; ambapo tangu siku ya Jumantatu iliyopita na baada ya kumalizika muda uliotolewa na muqawama kwa Tel Aviv kuhakikisha umekomesha uvamizi wake dhidi ya Quds na msikiti wa Al Aqsa, mapambano baina ya pande mbili hizo yamezidi kupamba moto.../

Tags