May 15, 2021 04:30 UTC

Siku kadhaa zimepita tangu kuanza vita vya Israel na muqawama wa Palestina vinavyojulikana kwa jina la "Saifel Quds" na ingawa kutokana na ukatili wake usio na kifani, utawala wa Kizayuni unasababisha hasara kuwba za roho na mali za Wapalestina kwa kushambulia makazi ya watu, lakini vita hivyo ni kengele ya hatari kwa Israel kwa ushahidi mbalimbali.

Nukta ya kwanza kabisa inayohusiana na vita hivyo, ni kiwango kikubwa sana cha maroketi na makombora yaliyorushwa na wanamapambano wa Palestina dhidi ya maeneo nyeti na muhimu ya Wazayuni, katika siku chache tu za tangu kuanza vita hivyo.

Licha ya kuchuja mno habari, lakini pamoja na hayo, jeshi la utawala wa Kizayuni limetangaza kuwa, Wapalestina wameyapiga maeneo ya Wazayuni kwa makombora na maroketi 1,500 katika kipindi cha siku 3 tu za tangu kuanza vita hivyo.

Abu Ubaidah, msemaji wa Brigedi za Izzuddin al Qassam, tawi la kijeshi la Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS ametangaza pia habari ya kutumiwa kwa mara ya kwanza kombora la masafa ya kati liitwalo Ayyash na kupiga uwanja wa ndege wa Ramon wa utawala wa Kizayuni ambao uko umbali wa kilomita 220 kutoka Ukanda wa Ghaza. Kombara hilo la Ayyash lina uwezo wa kupiga shabaha ya umbali wa kilomita 250 na lina uwezo mkubwa wa kusambaratisha eneo linapopiga. Wanamapambano wa Palestina aidha wametangaza wazi kwamba wamejiandaa kwa vita vya muda mrefu.

Wanamapambano wa Palestina wakijiandaa kurusha droni ya kupiga maeneo nyeti ya Wazayuni

Tangu mwaka 2006, utawala wa Kizayuni umelizingira eneo la Ghaza kila upande, kuanzia angani hadi ardhini na hadi baharini. Mzingiro huo umetoa fursa kwa makundi ya muqawama kufanya tafiti na juhudi za kujitosheleza kijeshi, na hilo ni tishio kubwa kwa uwepo wa Israel.

Nukta ya pili muhimu ni kuhusu idadi ya Wazayuni wanauwa na makumi ya wengine wanaojeruhiwa kutokana na mashambulio ya wanamuqawama wa Palestina. Maeneo yote ya utawala wa Kizayuni sasa hivi yanaishi katika hofu kubwa. Wazayuni wanakimbilia kwenye mahandaki, maisha yamewaharibikia, huku mfumo wa kujilinda kwa makombora unaoitwa "Ngao ya Chuma" ukizidi kuonesha udhaifu wake wa kukabiliana na maroketi na makombora ya wanamapambano wa Palestina.

Kufeli huko kwa "Ngao ya Chuma" ya Israel kukabiliana na makombora na maroketi ya wanamapambano wa Palestina kunaweza kuchambuliwa katika sura mbili. Kwa upande mmoja mfumo huo wa kujilinda na mashambulizi ya makombora hauwezi kukabiliana na wimbi kubwa la makombora yanayovurumishwa kwa mkupuo mmoja kutoka Ghaza. Pili, utumiaji wa mfumo huo unautia hasara kubwa ya kifedha utawala wa Kizayuni. Taarifa zilisosambawa na gazeti la Kizayuni la 'Israel Hayom' zinasema kuwa, kila kombora moja linalovurumishwa na "Ngao ya Chuma" linaigharimu Israel dola 80 elfu. Kwa kweli Wazayuni wanalazimika kutumia makumi ya maelfu ya dola kukabiliana na kombora na roketi la wanamapambano wa Kiislamu wa Palestina, wakati gharama na roketi na kombora hilo la wanamamuqawama wa Palestina hadi kufyatuliwa kwake, ni ndogo mno; ni dola elfu chache tu.

Makombora ya Wanamapambano wa Palestina ni jinamizi kwa uwepo wa utawala wa Kizayuni wa Israel

 

Nukta ya tatu ni kwamba, katika vita vya hivi sasa, tofauti na huko nyuma, makundi ya muqawama wa Palestina yameonesha uwezo mkubwa wa kupiga kwa kina maeneo ya kiistratijia ya Israel kama vile viwanja vikubwa vya ndege. Katika siku chache tu za tangu kuanza vita vya "Saifel Quds" makundi ya muqawama ya Palestina yamelazimisha kufutwa safari za ndege za uwanja wa ndege wa kimataifa wa Ben Gurion huko Telaviv. Wazayuni walikusudia kuutumia uwanja wa ndege wa kimataifa wa Ramon uliko umbali wa kilomita 220 kusini mwa Ukanda wa Ghaza baada ya kushambuliwa ule wa Ben Gurion. Hata hivyo, uwanja huo wa ndege wa Ramon nao umepigwa kwa kombora jipya la Ayyash lenye uwezo wa kupiga umbali wa kilomita 250 na kulazimisha kufutwa safari za ndege za uwanja huo pia. 

Kiujumla hasara unazopata utawala wa Kizayuni katika vita vya hivi sasa ni nyingi sana na ni za kila upande kiasi kwamba, chama cha wazalishaji bidhaa cha utawala wa Kizayuni kimetangaza kuwa, katika kipindi cha siku tatu za tangu yalipoanza mashambulizi ya makombora wanamapambano wa Palestina, sekta ya uzalishaji bidhaa ya Israel ilikuwa imeshapata hasara ya dola miliioni 160.

Shirika la habari la FARS lilinukuu taarifa ya chama hicho cha wazalishaji bidhaa cha Wazayuni kikiri juzi Alkhamisi kuhusu hasara kubwa iliyosababishwa na mashambulio ya makombora ya wanamapambano wa Palesitna na kuongeza kuwa, sekta mbalimbali za uchumi wa Israel zimepata hasara kubwa katika mashambulizi tangu siku tatu za kuanza kushambuliwa maeneo mbalimbali ya utawala wa Kizayuni kwa makombora ya wanamapambano wa Palestina.

Tags