May 15, 2021 07:38 UTC
  • Jinai mpya za Wazayuni; Israel yaua kwa umati familia ya watu saba Ghaza

Utawala wa Kizayuni unaendelea kufanya jinai za kinyama na za kutisha dhidi ya Wapalestina. Habari za karibuni kabisa zinasema kwamba utawala huo katili umeua kwa umati familia ya watu saba magharibi mwa mji wa Ghaza katika shambulio lake la anga. Watu hao waliouliwa kikatili na Wazayuni ni wanawake watano na watoto wadogo wawili

Shirika la habari la SAFA limeripoti kuwa, alfajiri ya leo Jumamosi, ndege za kivita za Israel zimeshambulia nyumba ya rais mmoja wa Palestina aitwaye Abu Hatab katika kambi ya wakimbizi wa al Shati na kuua kwa umati watu 7 wa familia moja.

Duru nyingine za Palestina zimetangaza habari ya kushambuliwa boti za Wapalestina na jeshi la utawala wa Kizayuni.

Habari za karibuni kabisa za maafa ya roho za Wapalestina yaliyosababishwa na mashambulio ya kikatili ya Wazayuni zinasema kuwa, Wapalestina 126 wameshauawa wakiwemo watoto 31 na wanawake 20. Wapalestina wengine zaidi ya 900 wameshajeruhiwa hadi hivi sasa.

Hali si shwari pia katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan

 

Jinai hizo za utawala wa Kizayuni zinafanyika kwa baraka na msaada kamili wa madola ya Magharibi kiasi kwamba waziri mkuu wa utawala huo haramu, Benjamin Netanyahu; amewashukuru na kuwapongeza marais Joe Biden wa Marekani na Emmanuel Macron wa Ufaransa, Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson na Kansela Angela Merkel wa Ujerumani kwa kuunga mkono utawala huo dhalimu katika jinai unazoendelea kufanya dhidi ya wananchi madhulumu wa Palestina.

Netanyahu ametoa shukrani hizo sambamba na kutoa vitisho kwa mara nyingine tena dhidi ya makundi ya muqawama ya Palestina kwa kueleza kwamba, utawala wa Kizayuni utatoa pigo kali kwa makundi hayo.

Kwa upande wake, msemaji wa harakati ya Jihadul Islami, Abu Hamza, amejibu vitisho hivyo vya Netanyahu  kwa kusisitiza kuwa, mapambano ya nchi kavu ni njia ya mkato zaidi kwa muqawama kufikia ushindi na kwamba katika mapigano hayo, hatima ya wanajeshi wa Kizayuni itakuwa ni ima kutekwa au kuuawa.

Tags