May 15, 2021 13:44 UTC
  • Al Houthi: Badala ya Yemen, Saudia iushambulie utawala wa Kizayuni unaowavurumishia makombora Wapalestina

Mjumbe wa Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen ameitaka Saudi Arabia isimamishe mashambulio na uchokozi wake dhidi ya Yemen na badala yake ielekeze mashambulio hayo kwa utawala haramu wa Kizayuni wa Israel unaoyahujumu kwa makombora maeneo ya Wapalestina.

Muhammad Ali Al Houthi ameyasema hayo katika ujumbe alioandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter kufuatia mashambulio ya kinyama yanayoendelea kufanywa na utawala katili wa Kizayuni dhidi ya wananchi wa Palestina na kushindwa Saudia kuchukua hatua yoyote kuhusiana na jinai hizo.

Al Houthi amesema: Ninaitaka Saudi Arabia na muungano wake ziulenge utawala ghasibu wa Israel kwa mashambulio kadhaa ili taifa la Palestina lipate ushindi.

Mjumbe huyo wa Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen amebainisha kuwa, ikiwa Saudia itachukua hatua hiyo, Yemen nayo itafumbia macho haki yake ya kujibu mapigo kwa mashambulio, ijapokuwa mashambulio na mzingiro wa Riyadh na waitifaki wake dhidi ya nchi hiyo ungali unaendelea.

Hujuma za Saudia na waitifaki wake nchini Yemen

Tokea ulipoanza mwezi mtukufu wa Ramdhani hadi sasa, mji wa Baitul Muqaddas (Jerusalem) unaokaliwa kwa mabavu na baadhi ya miji mingine ya Palestina inashuhudia makabiliano kati ya askari wa utawala haramu wa Israel na waandamanaji na waumini Wapalestina wanaopinga mwendelezo wa jinai na njama za uyahudishaji zinazofanywa na utawala wa Kizayuni; ambapo tangu siku ya Jumatatu iliyopita na baada ya kumalizika muda uliotolewa na muqawama kwa Tel Aviv kuhakikisha umekomesha uvamizi wake dhidi ya Quds na msikiti wa Al Aqsa, mapambano baina ya pande mbili hizo yamezidi kupamba moto.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na shirika la ulinzi wa raia katika Ukanda wa Gaza, tangu yalipoanza mashambulio ya kinyama ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya eneo hilo, hadi sasa Wapalestina wasiopungua 139, wakiwemo watoto 39 na wanawake 22 wameuawa shahidi na wengine wasiopungua 950 wamejeruhiwa.../