May 15, 2021 14:22 UTC
  • Tel Aviv na Ashdod zashambuliwa kwa makumi ya makombora kujibu jinai ya mauaji ya halaiki ya Shat'i

Brigedi za Izzuddin al Qassam, tawi la kijeshi la Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS zimefyatua makumi ya makombora kulenga mji mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel, Tel Aviv na wa bandari wa Ashdod kujibu jinai ya mauaji ya halaiki yaliyofanywa na jeshi la utawala huo haramu katika kambi ya wakimbizi wa Kiplaestina ya Shat'i.

Brigedi za Al Qassam zimeeleza katika taarifa kuwa, makumi ya makombora yamefyatuliwa kuelekea Tel Aviv kujibu jinai ya mauaji ya umati dhidi ya watoto, wanawake na raia Wapalestina katika kambi ya Shat'i.

Wakati huohuo vyombo vya habari vya Kizayuni navyo pia vimeripoti kuwa, makombora yasiyopungua 30 yamefyatuliwa kuelekea Tel Aviv na maeneo ya kandokando yake huku baadhi ya duru zikitangaza kuwa ving'ora vya tahadhari ya hali ya hatari vimesikika katika mji huo.

Tawi la kijeshi la harakati ya Hamas limeripoti kuwa, makumi mengine ya makombora yamefyatuliwa kuelekea mji wa bandari wa Ashdod, ambao ni miongoni mwa vituo muhimu zaidi vya kibiashara vya utawala wa Kizayuni.

Wanamuqawama wa Izzuddin al Qassam

Ashdod ndio bandari kubwa zaidi ya utawala ghasibu wa Israel ambapo zaidi ya asilimia 60 ya bidhaa za Wazayuni zinaingizwa kupitia bandari hiyo.

Kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya Kizayuni, jeshi la utawala huo limewataka wakazi wa  Tel Aviv waelekee kwenye maficho yao na kusalia huko hadi litakapotolewa tangazo jengine.

Alfajiri ya kuamkia leo, ndege za kivita za utawala haramu wa Israel zilishambulia bila taarifa kambi ya wakimbizi wa ndani wa Palestina ya Shat'i iliyoko Ukanda wa Gaza. Katika shambulio hilo la kinyama lililolenga nyumba za raia wawili wa Palestina, watu 10 wa familia hizo wakiwemo watoto wadogo wanane na wanawake wawili waliuawa shahidi na wengine wasiopungua 15 walijeruhiwa.../