May 18, 2021 02:51 UTC

Maandamano makubwa ya kuliunga mkono taifa linalodhulumiwa la Palestina na mapambano yake ya ukombozi, yamefanyika huko San'a, mji mkuu wa Yemen.

Kwa mujibu wa televisheni ya al Alam, Ofisi ya Kisiasa ya Ansarullah ya Yemen ndiyo iliyoitisha maandamano hayo ambayo yameshirikisha mamia ya maelfu ya waungaji mkono wa ukombozi wa Palestina.

Ofisi hiyo imesema, mlingano wa kutoa majibu na kuzuia mashambulizi huko Palestina umevunja makadirio na tathmini za kivita, na sasa hivi umemtia adui Mzayuni katika wakati mgumu na hofu kubwa.

Wazayuni wanapotwangwa kwa makombora ya muqawama

 

Washiriki wa maandamano hayo ya jana walibeba mabango ya kulaani siasa za kieneo za Marekani, waliunga mkono kadhia muhimu zaidi katika ulimwengu wa Kiislamu hivi sasa yaani Palestina na kutoa bishara za ushindi usioepukika wa kambi ya muqawama. Waandamanaji hao pia wametoa kaulimbiu mbalimbali kama vile "hatushughulishwi na lawama za wenye kulaumu," "mwisho wa Israel umeanza kwa ukamanda wa Abu Jibril," "Itwangeni kwa makombora Tel Aviv na uchomeni kwa moto mji huo," "Marekani na Israel ndio maadui wetu hasa" na kaulimbiu kama hizo.

Katika tangazo la mwisho la maandamano yao, wananchi wa Yemen wamelaani jinai za kikatili na za kinyama za utawala wa Kizayuni dhidi ya wakazi wa Ghaza, Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na maeneo mengine ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu na Wazayuni na kusema, hasira za makombora mazito na makubwa zitawaangamiza Wazayuni makatili. Taarifa hiyo pia imesema, leo hii kusikika sauti za makombora ya muqawama ndani ya Tel Aviv na maeneo mengine ya mbali ni ushahidi wa kutimia ahadi ya Mwenyezi Mungu ya kuwa pamoja na wanaosubiri na ni funzo kwa umma mzima kwamba anayenusuru matukufu ya Mwenyezi Mungu, Yeye Naye humnusuru.