Jun 03, 2021 03:50 UTC
  • Serikali ya Paestina yataka kusitishwa ujenzi wa vitongoji vya walowezi unaofanywa na Israel

Wizara ya Mambo ya Nje ya Palestina imelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) kutekeleza majukumu yao mkabala na jinai za kila siku zinazofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel za kujenga vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Palestina.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Palestina pia imevita vyombo hivyo vya kimataifa vitekeleza maazimio yote yanayohusiana na suala hilo. Wizara hiyo imeeleza kuwa, inalaani uamuzi wa utawala ghasibu wa Israel wa kuanza kujenga nyumba 350 mpya kwa ajili ya walowezi wa Kizayuni katika mji wa Bet El karibu na mji wa Ramallah katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan katika fremu ya kupanua ujenzi wa vitongoji hivyo vya walowezi kwenye ardhi za Palestina.  

Wizara ya Mambo ya Nje ya Palestina imesema katika taarifa yake kuwa, lengo la kuanza ujenzi wa nyumba hizo za walowezi wa Kizayuni ni kupanua na kuimarisha mpango wa Israel wa kuziunganisha baadhi ya ardhi za Ukingo wa Magharibi mwa Mto Jordan na Quds Mashariki. Taarifa hiyo imeongeza kuwa utawala wa Israel ni mhusika kikamilifu wa jinai hizo za kujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi inayokaliwa kwa mabavu ya raia wa Palestina, kubomoa nyumba na kuwalazimisha raia wa Palestina kuyahama makazi yao. 

Nyumba za Wapalestina zikiwa zimebomolewa na Israel al Quds ya mashariki 

Kwa mujibu wa maazimio ya Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama la umoja huo, ujenzi wowote wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni ndani ya mipaka ya mwaka 1967 katika eneo la Ukingo wa Magharibi mwa Mto Jordan ni kinyume cha sheria.

Tags