Jun 06, 2021 02:26 UTC
  • Upinzani Bahrain wailaani US kupeperusha 'bendera ya ushoga' Manama

Chama kimoja cha upinzani nchini Bahrain kimekosoa vikali hatua ya Marekani ya kupeperusha bendera yenye nembo ya kuunga mkono ushoga katika ubalozi wake mjini Manama.

Muungano wa Vijana wa Harakati ya Februari 14 umetoa taarifa ukilaani vikali kitendo hicho, ambacho unasisitiza kuwa kinaenda kinyume na mafundisho ya Kiislamu na thamani za kimaadili za taifa hilo.

Taarifa hiyo imeeleza bayana kuwa, hatua ya Marekani kupandisha bendera yenye nembo ya kuunga mkono usenge na usagaji katika jengo la ubalozi wake mjini Manama ni tusi kwa matukufu ya Kiislamu na kwa utamaduni wa watu wa Bahrain.

Muungano wa Vijana wa Harakati ya Februari 14 umebainisha katika taarifa hiyo kuwa, kitendo hicho cha Marekani hakina malengo mengine ghairi ya kushajiisha ufuska na mmomonyoko wa maadili katika taifa hilo dogo la Ghuba ya Uajemi.

Kadhalika taarifa hiyo imeukosoa vikali utawala Aal-Khalifa kwa kunyamazia kimya uchafu huo ambao si tu umehujumu mafundisho ya Uislamu, lakini pia umeumiza hisia za wananchi wa Bahrain.

Maandamano ya Wabahain ya kupinga utawala wa Aal-Khalifa

Muungano wa Vijana wa Harakati ya Februari 14 umesisitiza kuwa, utawala wa Rais Joe Biden wa Marekani na balozi mdogo wa US mjini Manama, Maggie Nardi wanapaswa kufahamu kuwa, wananchi wa Bahrain na vikosi vya kimapunduzi havitafumbia macho kitendo hicho cha kihaini na kichokozi, na vinataka kuheshimishwa mila, tamaduni na desturi za Wabahrain.

Februari 14 mwaka huu 2021 ilisadifiana na kutimia mwaka wa 10 wa mapambano ya Februari 14 ya wananchi wa Bahrain dhidi ya utawala wa Aal-Khalifa, sambamba na kuanza mwaka wa 11 wa mapambano hayo.

Tags