Jun 12, 2021 02:52 UTC
  • Kwa nini Baraza Kuu la Kisiasa Yemen limetoa masharti matatu kwa ajili ya kufanikisha mazungumzo ya amani?

Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen limekaribisha jitihada za kukomesha mashaka na machungu ya taifa la nchi hiyo na kutangaza masharti matatu makuu kwa ajii ya mazungumzo yajayo ya kusaka amani.

Sambamba na kusisitiza misimamo thabiti ya Jamhuri ya Yemen ya kukaribisha fikra na ujumbe unaotambua rasmi mamlaka ya kujitawala nchi hiyo, baraza hilo limetangaza kuwa, mambo matatu yanapaswa kuzingatiwa katika mazungumzo yajayo, nayo ni kuondolewa mzingiro wa pande zote dhidi ya Yemen, kusitishwa mashambulizi ya aga, nchi kavu na baharini na kukomeshwa uvamizi pamoja na kuondoka wapiganaji wote wa kigeni katika ardhi ya Yemen na kusitisha uingiliaji wa nchi za kigeni katika masuala ya ndani ya nchi hiyo. 

Vita vya Saudi Arabia na washirika wake dhidi ya taifa la Yemen vinaendelea kwa kipindi cha miezi 75 sasa. Zaidi ya Wayemeni elfu 17 wameuwa moja kwa moja katika vita hivyo na makumi ya maelfu ya wengine wamejeruhiwa. Vyombo rasmi vya Yemen vimetangaza kuwa, zaidi ya raia laki moja wa nchi hiyo pia wameuawa kwa njia isiyo ya moja kwa moja kutokana na athari mbaya za vita na mashambulizi hayo ikiwa ni pamoja na maradhi ya kuambukiza yaliyosababishwa na vita, njaa na ukame. Umoja wa Mataifa pia umethibitisha kuwa vita hivyo vya Saudi Arabia na washirika wake dhidi ya taifa la Yemen vimesababisha maafa makubwa zaidi ya binadamu ambayo hayajawahi kushuhudia duniani katika miongo miwili ya karibuni ya karne ya 21. 

Saudi Arabia inaendelea kuua raia wa Yemen

Hapa linakuja swali kwamba, masharti yaliyotolewa na Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen kwa ajili ya kufanikisha mazungumzo yajayo ya amani yana maana gani?

Kwanza ni kwamba, vita dhidi ya taifa la Yemen si mashambulizi ya kila siku ya mabomu na makombora pekee. Ni kweli kwamba, zaidi ya Wayemeni elfu 17 wameuawa kwa mashambulizi ya ndege za kivita, mabomu na makombora ya Saudia na washirika wake, lakini inatupasa kuelewa kuwa, mzingiro wa pande zote wa wavamizi hao umesababisha vifo vya zaidi ya Wayemeni laki moja. Kwa msingi huo athari mbaya za mzingiro huo wa pande zote za nchi kavu, angani na baharini ni kubwa zaidi kuliko hata mashambulizi ya moja kwa moja ya ndege, makombora na mabomu ya Saudia na wavamizi wenzake. 

Katibu Mkuu wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon Sayyid Hassan Nasrullah aliashiria suala hilo katika hotuba yake ya Jumanne iliyopita na kusema: "Saudi Arabia na Marekani zinataka vita visitishwe lakini mzingiro dhidi ya taifa la Yemen uendelee kama ulivyo." Ni kwa msingi huo ndiyo maana serikali ya Uokovu wa Kitaifa nchini Yemen inasisitiza kuwa, kusitishwa vita bila ya kukomeshwa mzingiro wa Yemen hakutakuwa na maana yoyote. 

Pili ni kwamba, maana ya masharti hayo ni sisitizo la Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen kuhusu umuhimu wa kujitawala na mamlaka ya nchi hiyo. Itakumbukwa kuwa, baada ya kuivamia Yemen, Saudi Arabia na Imarati zilikalia kwa mabavu baadhi ya maeneo ya nchi hiyo, suala ambalo linakiuka mamlaka ya kujitawala ya nchi hiyo. Kwa msingi huo, kusitishwa vita vya Yemen bila la kuondoka askari na wapiganaji wa kigeni katika ardhi ya Yemen kutakuwa na maana ya kuendelea kukaliwa kwa mabavu nchi hiyo na hata kugawika katika pande kadhaa. Suala hilo halikubaliwi na Serikali ya Uokovu wa Kitaifa ya Yemen inayosisitiza umoja wa ardhi yote ya nchi hiyo. 

Wapiganaji wa Ansarullah

Tatu ni kwamba, maana ya masharti hayo ni kuwa, katika medani za vita Wayemeni wana uwezo wa kuitia hasara kubwa zaidi Saudia na waitifaki wake. Kwa upande mmoja, Saudia inakabiliwa na mashinikizo ya walimwengu kutokana na jinai za kivita na jinai dhidi ya binadamu zilizofanyika huko Yemen, na katika upande wingine ina wasiwasi kuhusu mashambulizi ya jeshi na wapiganaji wa kujitolea wa Yemen dhidi ya nchi hiyo. Hivyo, japokuwa Serikali ya Uokovu wa Kitaifa ya Yemeni inakaribisha mazungumzo ya amani, lakini Saudi Arabia inaonekana kutaka zaidi mazungumzo hayo kwa ajili ya kujinasua katika kinamasi cha Yemen. 

Nukta ya mwisho ya kuashiria hapa ni kuwa, masharti matatu yaliyotolewa na Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen ni sisitio la kujitawala, ardhi kamili na moja ya Yemen na mamlaka ya kujitwala nchi hiyo; na hapana shaka kuwa, kutimizwa masharti hayo kutakuwa na maana ya ushindi wa taifa la Yemen katika vita hivyo vya kulazimishwa. 

Ni kwa kuzingatia hayo yote ndiyo maana Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen likatangaza kuwa, nchi hiyo inakaribia kupata ushindi.