Jun 12, 2021 04:12 UTC
  • Mahmoud al Zahar
    Mahmoud al Zahar

Mwanachama mwandamizi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) amesema katika mapambano ya siku 12 hivi karibuni, harakati za ukombozi wa Palestina zimetoa pigo kubwa kwa nadharia ya usalama ya utawala wa Kizayuni wa Israel ambayo imejengeka kwa msingi kuwa utawala huo una uwezo zaidi ya wote katika eneo.

Katika mahojiano na televisheni ya Al Mayadeen siku ya Ijumaa, Mahmoud al Zahar amsema maslahi ya pamoja ya Syria, Lebanon, na Palestina ni kuushinda utawala wa Kizayuni wa Israel. Amesema ili kufikia lengo hilo kuna haja ya ushirikiano wa pande zote kwa msingi wa kuuangamiza utawala huo wa Kizayuni na kukomboa ardhi zote za Palestina.

Amesema baada ya Wapalestina wanaoishi katika ardhi zilizokaliwa kwa mabavu 1948 na Quds Tukufu kutambua majukumu yao na uwezo wao wa kujihami na kutetea haki zao, vita vijavyo vitaainisha hatima.

Wapalestina 253 waliuawa shahidi katika vita vya siku 12 vilivyoanzishwa na utawala wa Kizayuni wa Israel huko Ukanda wa Ghaza mwezi Mei mwaka huu. Watoto 66, wanawake 39 na wazee 17 ni miongoni mwa raia wa Palestina waliouliwa shahidi katika vita hivyo vya Israel. Wapalestina wengine zaidi ya 1900 walijeruhiwa katika mashambulizi hayo ya kinyama dhidi ya Ghaza. 

Tags